Saturday, 28 August 2021

MPANGO WA USIMAMIZI WA MAZINGIRA WILAYA ZA SINGIDA MBIONI KUKAMILIKA

Mratibu wa Sera kutoka Shirika la Kuendeleza Kilimo Hai nchini (TOAM), Paul Chilewa, akizungumza katika kikao kilicho wakutanisha wataalam kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Wizara ya Kilimo, TAMISEMI, na Mashirika ya kuendeleza Kilimo Hai nchini (TOAM, GIZ na Helvetas), ambacho kilifanyika juzi mkoani hapa lengo likiwa ni kutathmini na kuweka mikakati ya kuhakikisha ajenda ya 'Kilimo Himilivu' na 'Mabadiliko ya Tabianchi' vinaingizwa katika Mpango wa Mazingira wa miaka mitano ndani ya halmashauri za wilaya za Singida.

Washiriki wakiwa kwenye kikao hicho.

Mratibu wa Mradi wa Kilimo Himilivu cha Pamba kutoka GIZ kwa mkoa wa Singida, Leonard Mtama, akichangia jambo kwenye kikao hicho.

Kikao kikiendelea.
Afisa Kilimo kutoka Wilaya ya Mkalama,  Seleman Musunga, akizungumza kwenye kikao hicho.
Afisa Mazingira kutoka Wilaya ya Iramba, Yohana Dondi,akizungumza kwenye kikao hicho.

Washiriki wa kikao hicho wakiwa katika picha ya pamoja,
Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Singida.


WATAALAMU mbalimbali wamekutana kutathmini na kuweka mikakati ya kuhakikisha ajenda ya 'Kilimo Himilivu' na 'Mabadiliko ya Tabianchi' vinaingizwa katika Mpango wa Mazingira wa miaka mitano ndani ya halmashauri za wilaya za Singida ili kuwezesha kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi sambamba na kuongeza tija katika kilimo.

Kupitia kikao hicho wataalam hao kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Wizara ya Kilimo, TAMISEMI, na Mashirika ya kuendeleza Kilimo Hai nchini (TOAM, GIZ na Helvetas), pamoja na mambo mengine, walijikita katika kuziwezesha halmashauri mkoani hapa kutengeneza mipango inayoweza kuratibu na kusimamia uharibifu wa mazingira kwenye maeneo yao.

Mratibu wa Sera kutoka Shirika la Kuendeleza Kilimo Hai nchini (TOAM), Paul Chilewa, alisema wamekutanisha  wilaya nne za Manyoni, Ikungi, Iramba na Mkalama ndani ya mkoa wa Singida ili kuzisaidia kitaalamu kutengeneza mipango hiyo ambayo inakwenda kuanza kutumika katika kipindi cha miaka 5.

Alisema lengo la TOAM ni kuhakikisha kwenye mpango huo masuala yote ya Kilimo Himilivu  na Mabadiliko ya Tabianchi yanaingizwa kikamilifu ili kuongeza tija kwenye kilimo katika muktadha chanya wa ongezeko la uzalishaji, ubora na zaidi kuifanya ardhi kuwa endelevu kwa matumizi ya kizazi cha sasa na baadaye.

Chilewa ambaye anatoka kwenye shirika hilo ambalo ni mwamvuli wa mashirika yenye lengo la kuendeleza kilimo hai nchini alisema mathalani kama taifa litajikita kwenye kuzalisha zao la Pamba kwa mfumo wa 'Kilimo Hai' na kuweka sera madhubuti sio tu litapata faida kubwa lakini pia wananchi wote wanaolima zao hili na mengine ya chakula kwenye eneo hilo watakuwa na uhakika wa kupata ithibati ya kuuza mazao yao kwenye soko la dunia kutokana na matokeo ya ubora wake.

"Uzalishaji wa pamba ya kilimo hai kwenye maeneo mengine duniani zikiwemo nchi za Afghanistan na India kwasasa kuna changamoto,  hivyo kama tutazalisha pamba hii (Organic Cotton) tutapata faida kutokana na kuwa na mahitaji makubwa kwenye soko," alieleza Chilewa.

Alisema lengo la kikao hicho, pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha kunakuwa na mkakati ambao utahakikisha kilimo kinazingatia taratibu zote za kilimo himilivu kwenye mabadiliko ya tabianchi.

"Hapa tupo kimkoa lakini TOAM kwa kushirikiana na wenzetu GIZ Tanzania, Helvetas na wadau wengine ndani ya wilaya hizi za mkoa wa Singida tunataka kuzisaidia halmashauri kutengeneza mpango huu na kuchukua hatua ya kuwa na miradi mbadala ikiwemo kupanda miti na kuanzisha mashamba darasa ya kujifunzia hizi teknolojia kwa ustawi na tija," anasema.

Hata hivyo Chilewa alishauri kuangalia baadhi ya teknolojia na shughuli nyingine za kibinadamu zinazotumika katika kilimo hususani suala la matumizi makubwa ya mbolea za viwandani ambayo kwa kiasi kikubwa zinachangia kufanya mazingira yasiwe himilivu.

Katika hilo, alisema Tanzania ni nchi ya pili Afrika kwa wingi wa mifugo, lakini kitu cha kushangaza wakulima wake walio wengi hawatumii hizo mbolea za mifugo hususani ng'ombe katika kurutubisha ardhi.

Alisema hata zile teknolojia na aina nyingine za mbolea ambazo zinaweza kurutubisha ardhi kwa kiwango cha kutoathiri- kwa maana ya kuifanya ardhi iendelee kuishi na kuzalisha nazo bado hazitiliwi mkazo wala kutumika ipasavyo.

Chilewa zaidi aliainisha baadhi ya viashiria vya uharibifu huo wa mazingira kuwa ni pamoja na matumizi yasiyo sahihi ya maji, wingi wa mifugo isiyozingatia tija, ukataji miti hovyo na uchomaji mkaa sambamba na matumizi makubwa ya viuatilifu ambavyo vina athari kwa udongo na afya za watu

"Hivyo kusanyiko la wadau na wataalamu hawa linalenga kutengeneza mpango wa miaka 5 utakaojibu changamoto hizi kwa kizazi cha sasa na kijacho katika muktadha wa kuwa na ufugaji endelevu na kilimo endelevu ambavyo vitazingatia utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi," alisema Chilewa.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Kilimo Himilivu cha Pamba kutoka GIZ kwa mkoa wa Singida, Leonard Mtama, kupitia kikao hicho anasema lengo lao hasa ni kusimamia na kuratibu utekelezaji wa mradi huo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

"GIZ tunaratibu tu hizi shughuli kwa pamoja na wenzetu wa TOAM, Helvetas, Tari, Kampuni ya Biosustain, Bodi ya Pamba na wadau wengine, lakini pia tunasimamia uboreshaji wa AMCOS kwa kushirikiana na Chuo cha Ushirika Moshi na tawi lake la Singida," alisema Mtama.

Alisema majukumu mengine ya shirika hilo, pamoja na mambo mengine, ni kuangalia kwa namna gani vikundi vya akinamama kupitia Helvetas vinaweza kujiongezea kipato kwa kuzalisha pamba hai na mazao mengine.

Kwa mujibu wa Mtama jukumu lingine la GIZ ni kuunganisha wazalishaji wadogo waliopo mkoa wa Singida na masoko ya ndani na nje lakini masharti ni kwamba mazao husika yatokane na kilimo hai.

"Hivyo sisi tunaratibu hayo mambo mawili uzalishaji wa mazao ya wakulima yaani pamba hai na mengine ya chakula kama Dengu, Choroko, alizeti na ufuta ili kuhakikisha uzalishaji wake unakuwa wa tija," anasema Mtama.

Katika hatua nyingine, alihimiza kuwa na azma ya pamoja ya kudumisha suala la ushirikiano kwa Idara, Taasisi na wadau wote kwenye kutunza mazingira huku akisisitiza juu ya umuhimu wa kila mmoja kwa nafasi yake mahali alipo kuchukua hatua katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.

"Unapotaka kufuga pia unapaswa kuangalia tija mfano badala ya kufuga ng'ombe 10 wenye kilo 50 kila mmoja ni bora ufuge kisasa ng'ombe mmoja mwenye kilo 500," alisisitiza Mtama.

Naye Afisa Maliasili na Mazingira mkoa wa Singida, Charles Kidua, alisema kama mkoa wamenufaika vilivyo na uwezeshaji wa wataalamu hao katika kutengeneza mipango hiyo ya usimamizi wa mazingira, na anaamini pale itakapoanza kutumika itasaidia kwenye usimamizi thabiti mazingira.

"Kikao hiki kimetuwezesha kutengeneza mipango mtambuka ya usimamizi mzuri wa mazingira kwenye eneo la misitu, kilimo, afya na maeneo mengine mengi kwa kuzingatia suala la mazingira ni jambo mtambuka," alisema Kidua. 

No comments:

Post a Comment