Friday, 27 August 2021

MAAFISA MAENDELEO JIJI LA ARUSHA WAKWAMISHA MIKOPO YA HALMASHAURIMaafisa Maendeleo ya Jamii wameonywa  kuacha tabia ya kudai vikundi vinavyotaka mikopo  ya asilimia kumi inayotolewa na halmashauri ya Jiji la Arusha kuwa  havijakidhi viwango badala yake watoe elimu juu ya mikopo wanayotoa  sanjari na urejeshwaji wa fedha kwa wakati.

 

Hayo yamejiri kwenye ziara ya Kamati ya Siasa Wilaya chini ya  Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Arusha Mjini, Joseph Massawe wakati wa ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kupitia ilani ya chama cha Mapinduzi na kuhakikisha  wananchi wanatatuliwa kero zao.


Massawe alisema ni aibu kwa maafisa maendeleo ya jamii kuwaambia wanavikundi kuwa vikundi vyao havijakidhi viwango badala yake wanapaswa kuwaelekeza jinsi ya kujaza fomu,mihuri na kuandika katiba.


Alihoji kushindwa kupata mikopo kwa vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu kunapelekea manung'uniko kwa wananchi na kuonekana kuna upendeleo katika utoaji wa fedha hizo au maafisa maendeleo ya jamii kata na Jiji kuwa kitu kimoja katika kuwanyima wanavikundi kupata mikopo.


"Hapa daraja mbili kunanini mbona awali vikundi vilikuwa vikipata mikopo lakini sasa hivi vikundi 18 vilivyoomba mkopo havijapata eti sababu hawajaanda katiba vizuri au wamekosa mihuri ya mwanasheria la wamekosea kuandika sasa wananchi wakikosea nyie wataalam si mpo acheni hizi tabia na ikigundulika mnahujumu zoezi la utoaji mikopo au kuendelea vikundi  mtachukuliwa hatua"


Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Wilaya ya Arusha Mjini,Mary Kisaka alihoji kwanini wanavikundi wakose mikopo ilhali wameshakamilisha taratibu zote zinazotakiwa na kusisitiza kunahujuma zinafanywa na afisa Maendeleo ya Jamii Jiji la Arusha,Mwanamsiu Dossi na Afisa Maendeleo Kata ya Daraja Mbili,Cresensia Shine


Ambapo Dossi alipopewa nafasi ili aeleze kwanini wanavikundi hao 18 wakose mikopo au kutokidhi vigezo alisema hana taarifa za vikundi hivyo huku Afisa maendeleo wa jamii kata hiyo shine alisema vikundi vitatu tu ndio vipo katika hatua ya kupata mikopo sababu vilitangulia awali lakini vikundi 18 bado havijapata mikopo kutokana na changamoto za mihuri ya wanasheria,kubadilika kwa kanuni za mikopo na ukosefu wa elimu juu ya marejesho.


Wakati huo huo,Mkuu wa Wilaya ya Arusha,Sophia Mjema alisisitiza kuwa elimu zaidi inahitajika kutolewa kwa vikundi mbalimbali na kuongeza kuwa kuanzia sasa ofisi yake kupitia wanasheria waliopo watawapigia mihuri wanavikundi wanaotaka mikopo ya halmashauri ili kuondoa usumbufu wanaopata wanaohitaji mikopo au kusajili vikundi vyao na kupata katiba.


Awali baadhi ya wanavikundi,Bhoke Magori na Asnatito Ismail wakazi wa daraja mbili walisema linapokuja suala la mikopo ya halmashauri wanapata shida ya kusajili vikundi,mihuri ya wanasheria,utengenezaji wa katiba ya kikundi na hata wakikamilisha ujazaji wa fomu wanaelezwa vikundi vyao kutokidhi vigezo wakihoji ni vigezo gani majibu hakuna na hatimaye wananchi kuona kama kunaupendeleo wa utoaji wa mikopo hivyo ni vyema suala hilo likaangaliwa kwa undani kwani kunaupendeleo wa utoaji mikopo kwa vikundi mbalimbali.

No comments:

Post a Comment