Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka akizungumza katika mkutano wa pamoja baina ya Viongozi wa Mkoa huo na Wafanyabiashara wadogo wadogo.Mmoja wa Wafanyabiashara wadogo wa Jiji la Dodoma aliyetambulika kwa jina la Dangote akitoa maoni yake kwenye mkutano wa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka.
Wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma wakiwa wanamsikiliza Mkuu wa Mkoa, Anthony Mtaka katika mkutano wa pamoja uliolenga kutatua changamoto za wafanyabiashara hao.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amewaruhusu wajasiriamali wa Jiji la Dodoma kufanya biashara zao hadi usiku huku akiahidi kuwaboreshea miundombinu.


RC Mtaka ameyasema hayo jijini Dodoma alipokua akizungumza na wafanyabiashara wadogo wadogo ambapo ameahidi Serikali ya Mkoa itashughulikia changamoto ya taa za Barabarani pamoja na kuhakikisha ulinzi wa uhakika unakuepo masaa yote.

Ametoa kauli hiyo alipokua akijibu swali la mmoja wa wamachinga hao aliyeomba kuongezewa kiwango cha muda wa kufanya Biashara zao, ndipo RC Mtaka aliporuhusu kufanya biashara zao hadi asubuhi.

" Hili eneo la Nyerere Square ambalo mnafanyia biashara hatuwezi kuwaongezea muda kama mnavyotaka muwe mnaanza kufanya biashara asubuhi, hatufanyi hivyo kwa kuwa hili ni eneo la Barabara ndio maana tukatoa kibali muwe mnaanza biashara zenu hapa jioni.

Lakini sasa kwa kuwa Dodoma ni Jiji tutaufanya mchana kuwa mrefu zaidi ya usiku kwa maana sasa mnaweza kufanya biashara zenu hadi asubuhi, niwaahidi tutaboresha miundombinu ya taa na patrol ya Polisi itakua inapita kuhakikisha usalama upo muda wote," Amesema RC Mtaka.

Aidha RC Mtaka pia amewataka wafanyabiashara hao wadogo wadogo kuzingatia sheria na kanuni za kufanya kwao biashara ili wasilete athari kwa wananchi wengine wakati wanatimiza majukumu yao.

RC Mtaka pia amewataka viongozi wa Serikali kuanzia mamlaka za chini kutokuwa kikwazo kwa wafanyabiashara hao na badala yake wawe sehemu ya kuwawezesha kukua kibiashara na kufikia malengo yao.

Mkutano huo uliwahusisha Wafanyabiashara wadogo kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Tawala wa Mkoa Dk Fatma Mganga, Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Dodoma,Wakuu wa Wilaya na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde.

Share To:

Post A Comment: