Tuesday, 20 July 2021

MSANDO ATAKA WADAU WA ELIMU WASAIDIWE NA SERIKALI


Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini, Albert Msando amewaagiza watendaji wa halmashauri ya manispaa hiyo, kushirikiana na wadau wa elimu kutatua changamoto ya miundombinu ya maji na upungufu wa vyumba vya madarasa shuleni, inayosababisha kushuka kwa kiwango cha elimu katika baadhi ya shule wilayani humo.
Msando ametoa agizo hilo baada ya kuzindua mradi wa kisima cha maji chenye ujazo wa lita elfu kimu uliofadhiliwa na Taasisi ya Elimu ya EGG Tanzania, kwenye shule ya sekondari Lupanga iliyopo wilayani humo.

Mkuu huyo amebainisha kuwa  kila mwaka Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya elimu bila malipo kwa watoto wa kitanzania hivyo  taasisi za kiraia zinapojitokeza kuunga mkono juhudi hizo ni vyema kupewa ushirikiano.

"Hatutawafumbia macho  wote watakao bainika kukwamisha juhudi za wadau wa elimu ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakishirikiana na Serikali katika nyanja mbalimbali kusukuma mbele maendeleo ya Elimu ya nchini,"-amesema mkuu huyo.

Aidha Msando amewataka wazazi na walezi kushirikiana na walimu katika kuwasaidia watoto kupenda kusoma ili kuleta matokeo chanya katika taaluma.

"Makambi yana umuhimu wake katika kuwaandaa wanafunzi kwenye mitihani yao ya Mwisho hivyo wazazi muwe msatari wa mbele kuwasadia watoto wenu kufanya vizuri kwenye masomo yao badala ya kutoa visingizio vya ukosefu wa pesa,"-amesisitiza Msando.

Naye Mkurugenzi wa Tasisi hiyo nchini Jumanne Mpinga,  amebainisha kuwa mradi huo  utakuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi  hususani watoto wa kike lakini pia jamii inayozunguka eneo la shule huku akiomba Serikali kuondoa tozo kwenye vibali vya kuchimba visima katika maeneo ya shule na Taasisi za Serikali.

No comments:

Post a Comment