MIKOA ya Arusha na Manyara imeongoza kwenye mchezo wa riadha meta 1,500 katika Michezo ya Shule za Sekondari Tanzania (Umisseta) kwenye fainali zilizofanyika Juni 30 mjini hapa.

Msemaji wa Umisseta 2021, John Mapepele amesema kwa upande wa wavulana, Daniel Patric kutoka Arusha aliibuka mshindi wa kwanza baada ya kumaliza mbio hizo kwa kutumia dakika 4:07:16 akifuatiwa na Paul Ndege kutoka mkoa wa Mara aliyetumia dakika 4:11:06, wakati nafasi ya tatu imechukuliwa na Agustino Leonard wa Manyara kwa dakika 4:12:44.

Kwa upande wa wasichana, Leoma Awaki kutoka Manyara ameibuka mshindi wa kwanza baada ya kumaliza mbio hizo kwa kutumia muda wa dakika 4:44:50 akifuatiwa na Esther Martin kutoka mkoa wa Pwani aliyetumia dakika 4:46:80, wakati nafasi ya tatu imechukuliwa na Nyanzobe Mbahi kutoka Mara.

Wakati huo huo, mkoa wa Unguja kwa upande wa wavulana umeibuka mshindi wa kwanza katika mbio za kupokezana vijiti meta 4x100 (relay) kwa kutumia sekunde 45:53, ukifuatiwa na mkoa wa Shinyanga 47:10, mkoa wa Tabora umeshika nafasi ya tatu kwa muda wa 47:20.

Kwa upande wa wasichana, mkoa wa Njombe umeibuka mshindi wa kwanza katika mbio za kupokezana vijiti meta 4x100 (relay) kwa kutumia sekunde 55:66, ukifuatiwa na mkoa wa Mara 56:16, mkoa wa Tabora umeshika nafasi ya tatu kwa muda wa 56:19.

Katika mchezo wa kuruka chini, mikoa ya Shinyanga na Pwani imetwaa ubingwa katika michezo hiyo jana.

Musa Yusufu kutoka Shinyanga ameibuka kuwa mshindi wa kwanza baada ya kuruka umbali wa meta sita na sentimeta 71 akifuatiwa na Mpaji Gipson kutoka mkoa wa Kigoma aliyeruka umbali wa meta sita na sentimita 35 wakati nafasi ya tatu imechukuliwa na Alexander Jumanne kutoka mkoa wa Geita.


Share To:

Post A Comment: