Monday, 12 July 2021

GEKUL: MACHO YA WATANZANIA YAPO NYUMA YENU

 

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul amewaambia wachezaji wa timu ya Taifa ya Riadha kuwa macho ya Watanzania na wapenda michezo wote yapo nyuma yao na wanamatumaini makubwa kwamba wataiwaikilisha vyema nchi yetu.

Mhe. Gekul ameyasema hayo leo tarehe 11 Julai, 2021 jijini Arusha wakati  alipowakibidhi wachezaji wa Timu ya Taifa ya Riadha bendera ya Taifa, vifaa vya michezo pamoja na tiketi za ndege.

Timu ya Taifa ya Riadha ipo kambini jijini Arusha ikijaanda na mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika nchini Japani mwezi Agosti, 2021.

"Macho yote ya Watanzania wapenda michezo yapo nyuma yenu yakiwatizama na kuwafuatilia kwa karibu kwa matumaini makubwa kwamba mtatuwakilisha vyema" - Mhe. Gekul

" Mmepata muda wa kutosha kujifua na kujiandaa kwa zaidi ya miezi miwili, Serikali inaimani kubwa kwamba mtarejea na medali hapa nchini" - Mhe. Gekul

Mhe. Gekul pia amewahakikishia wachezaji hao kuwa Serikali imekuwa bega kwa bega tangu kuanza kwa kambi na itaendelea kuiwezesha timu hiyo katika hatua zinazofuata ili iweze kufanya vyema katika mashindano hayo makubwa ya Kimataifa.

" Serikali imedhamiria kwa dhati kuendeleza michezo hapa nchini, na katika kudhihirisha hilo Wizara kupitia BMT imesaidia maandalizi ya kambi ya Timu hii pamoja na stahili nyingine za wachezaji watakapo kuwa nchini Japani" - Mhe. Gekul.

"Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa inazisaidia Timu za Taifa pamoja na vyama vya Michezo na Mashirikisho ili ziweze kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya Kimataifa kupitia mfuko wa Maendeleo ya Michezo ulioanzishwa" - Mhe. Gekul

Mhe. Gekul pia amevitaka vyama pamoja na Mashirikisho ya Michezo nchini kuzingatia utawala bora pamoja na kuratibu mashindano katika ngazi za mikoa na Taifa ili kuibua wacheza mahiri watakao iwakilisha nchi katika mashindano ya Kimataifa.

Timu ya Taifa ya Riadha iko kambini jijini Arusha ikijiandaa kushiriki mashindano ya Olimpiki nchini Japani ambapo wachezaji watatu wamefanikiwa kufuzu viwango vya Olimpiki ambao ni Felix Simbu, Failuna Matanga na Gabriel Geay.

Wachezaji hawa wanatarajia kuondoka nchini tarahe 27 Julai, 2021kuelekea nchini Japani kwaajili ya mashindano hayo.

No comments:

Post a Comment