Na Oscar Assenga, Tanga
Askofu Mkuu wa Kanisa la (FPCT) Tanzania, Stevie Mulenga, amewataka viongozi wa dini nchini, wakiwemo maaskofu, kutumia majukwaa ya kidini kuhubiri amani badala ya ujumbe unaoweza kuleta uchonganishi.
Askofu Mulenga alitoa wito huo leo wakati wa ibada ya Sikukuu ya Pasaka iliyofanyika katika kanisa hilo. Alisisitiza kuwa Yesu Kristo hakukuja kuleta uchonganishi, bali alikuja kuleta amani, hasa kupitia kufufuka kwake.
Alieleza kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuhubiri amani, upendo, uvumilivu na mshikamano miongoni mwa jamii, ili watu waweze kuishi kwa utulivu. Alisema huo ndio ushauri wake mkubwa kwa viongozi hao katika kipindi hiki cha Sikukuu ya Pasaka.
“Tunamshukuru Mungu kwa sababu haki ya kuabudu inaendelea kuheshimiwa nchini. Ingawa serikali haina dini, wananchi wake wana dini, na wanaendelea kuabudu bila kuvunja sheria. Wana uhuru mkubwa wa kuabudu mchana na usiku,” alisema Askofu Mulenga.
Aidha, aliwataka wananchi kulinda amani iliyopo na kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha fitina au vurugu. Alisisitiza kuwa ibada zinapaswa kuwa sehemu ya kufundisha neno la Mungu, siyo majukwaa ya kuchochea chuki au upendeleo kwa watu fulani.
Kwa upande mwingine, Askofu Mulenga alisema chanzo kikubwa cha mmomonyoko wa maadili ni tamaa binafsi, ambazo husababisha matukio mbalimbali yanayoshangaza hata jamii ya kimataifa.
Aliongeza kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuwaelimisha waumini wao juu ya kuepuka ukatili wa kijinsia, huku wakisisitiza umuhimu wa kuishi kwa amani, utulivu na kufuata matendo mema.

Post A Comment: