NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) wamekamata magari mawili yaliyokuwa yamepakia mazao kwa kutumia magunia yenye uzito unaozidi kipimo kinachoruhusiwa, katika operesheni ya kushtukiza iliyofanyika katika masoko ya Ilala na Temeke, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 4, 2026, Meneja wa WMA Mkoa wa Ilala, Muhono Nashon, amesema magari hayo yalibeba magunia yenye uzito wa kati ya kilo 170 hadi 200, kinyume na uzito rasmi usiozidi kilo 100 kwa kila gunia.

Amesema kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria za vipimo na kinaathiri haki ya wafanyabiashara pamoja na watumiaji.

“ Uzito unaotakiwa ni usiozidi kilo 100 kwa kila gunia, lakini tumekuta baadhi ya magunia yamezidi hadi kilo 200, jambo ambalo si sahihi,” amesema Nashon.

Nashon ameeleza kuwa wafanyabiashara waliokutwa na makosa wamepewa elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia vipimo sahihi, huku akisisitiza kuwa zoezi hilo litaendelea kufanyika mara kwa mara ili kudhibiti ukiukwaji huo.

Ameongeza kuwa ukaguzi huo hufanyika kwa kushtukiza kuanzia mashambani hadi masokoni kwa kushirikiana na halmashauri, hasa wakati wa upakiaji wa mazao na ukusanyaji wa ushuru.

Kwa mujibu wa sheria, amesema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukiuka taratibu hizo, ikiwemo faini kwa wanaokiri makosa au kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.

Kwa upande wake, mfanyabiashara wa viazi vitamu katika Soko la Temeke, Fatie Ally, amesema changamoto ya uelewa mdogo kuhusu viwango sahihi vya vipimo inachangia wafanyabiashara wengi kupakia mazao kwa kuzidisha uzito uliowekwa.

Amesema utoaji wa elimu ya kutosha kuanzia mashambani hadi masokoni utasaidia kupunguza tatizo hilo.

Nao wabeba mizigo (malumbesa) katika Soko la Ilala wameeleza kuwa kubeba magunia yenye uzito uliozidi kunawaathiri kiafya na kiuchumi, kwani hulipwa kwa viwango vinavyolingana na kilo 100 ilhali hubeba zaidi ya hapo.

“Changamoto ya maisha inatulazimisha kubeba mizigo bila kupima uzito wake. Unakuta gunia lina kilo 150 hadi 200 badala ya kilo 100 inayotakiwa,” amesema Issa Salum.

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: