Na. Benny Mwaipaja, Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) itekeleze haraka maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni kuhusu Taasisi za Fedha kupunguza riba za mikopo ili kuwawezesha wafanyabiashara na watanzania kwa ujumla kukopa na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Mhe. Masauni ametoa maagizo hayo alipotembelea Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Benki hiyo ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kutembelea Taasisi zilizochini ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Alipongeza jitihada zinazofanywa na Benki Kuu ya Tanzania za kukutana na wadau ili kuhakikisha kuwa Taasisi za Fedha zikiwemo Benki na Watoa huduma wa Sekta Ndogo ya Fedha wanapunguza riba za mikopo yao ili kuwawezesha wananchi kupata mikopo isiyo na gharama kubwa.

“Niwapongeze kwa juhudi zilizoanza kuchukuliwa kuwezesha riba kupungua na ikiwezekana mwishoni mwa mwezi huu wananchi waanze kuona matokeo ya juhudi hizo kwa riba kuanza kupungua, kwa kuwa kupungua kwa riba ni jambo linalowezekana”, alieleza Mhandisi Masauni.

Aidha, ameitaka Benki hiyo kuhakikisha inaweka mikakati mahususi ya kuongeza akiba ya Fedha za kigeni kwa kuwa na mbinu za kibunifu zikiwemo kuanza kununua na kuhifadhi dhahabu pamoja na kuongeza uuzaji wa bidhaa za Tanzania nje ya nchi na kusimamia kikamilifu shughuli za utalii.

Kuhusu suala la fedha za wananchi waliokuwa wateja wa Benki ya FBME Limited iliyowekwa chini ya uangalizi wa Bima ya Amana za Wateja inayosimamiwa  na Benki Kuu ya Tanzania ikiwa katika hatua za kufilisiwa, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Yussuf Masauni, ameitaka Benki hiyo kuhakikisha wateja wa Benki hiyo wanarejeshewa fedha zao haraka baada ya kukamilisha taratibu za kisheria zinazoendelea nchini Cyprus.

Kwa upande wake Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Bernard Kibesse, alimhakikishia Mhe. Naibu Waziri Masauni kwamba Benki yake inakamilisha mazungumzo na mabenki ili washushe riba kama alivyoelekeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan jijini Mwanza.

Alisema Benki Kuu pia inaendelea kurekebisha kanuni mbalimbali za mikopo inayotolewa na Benki hiyo kwa Mabenki ili kuziongezea ukwasi Benki hizo ili na zenyewe zitumie fursa hiyo kushusha riba za mikopo.

Aidha, Naibu Gavana Dkt. Kibese alieleza kuwa Benki Kuu ya Tanzania itaanza kununua na kuhifadhi dhahabu baada ya Kiwanda cha kuchakata dhahabu cha Mwanza kilichozinduliwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan jijini Mwanza hivi karibuni kupata hati ya uthibitisho ya uzalishaji wa dhahabu wa viwango vya kimataifa ambavyo ili cheti hicho kitolewe, kiwanda kinatakiwa kuzalisha dhahabu yenye ubora wa asilimia 99.9.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhandisi Masauni yupo jijini Dar es Salaam katika ziara yake kikazi ambapo atatembelea ofisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Share To:

Post A Comment: