NA HERI SHAABAN (MOROGORO)


MAMLAKA za Serikali za Mitaa zimetakiwa kutenga bajeti kwa ajili ya utoaji elimu  na usimamizi wa huduma za ustawi wa Jamii.



Hayo yalisemwa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Morogoro Bi. Jesca Kagunila wakati wa kikao kazi cha siku moja cha kuwajengea uwezo mafisa Ustawi wa Jamii wa halmashauri zote za Mkoa huo  kilichoandaliwa na Mkoa kwa kushirikiana na Mdau wa Mradi wa Kizazi kipya Kanda ya Kati kupitia Shirika la PACT TANZANIA



Akizungumza katika kikao kazi hicho Afisa Ustawi wa Jamii Jesca alisema Mamlaka za Serikali za Mitaa zitakapotenga bajeti ya kutosha Mamlaka rahisi  kusimamia masuala ya Ustawi ya Jamii bila kuwepo changamoto zozote katika sehemu zao za kazi na kuwawezesha kutoa huduma kwa weledi na  ufanisi


Jesca alisema  Maafisa Ustawi wa Jamii wamekuwa wakishughulika na Jamii hivyo watakapotengewa  bajeti ya kutosha itasaidia  kuifikia jamii  kwa ukubwa na wakati.


"Mamlaka za Serikali za Mitaa  zinatakiwa kuhakikisha vikao vya  mabaraza ya Wazee ,Watu Wenye Ulemavu na Kamati za kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto vinafanya kila robo kama ilivyoainishwa kwenye sera, sheria na miongozo" alisema Jesca .


Aidha aliwataka Maafisa Ustawi wa Jamii kuhakikisha takwimu za watoto ,wazee na watu wenye ulemavu zinahuishwa na utambuzi unafanyika kwa kuwashirikisha Watendaji wa Kata na Vijiji  pamoja na kujadiliwa kwenye vikao vya vijiji, kata na  halmashauri.


Pia wawe na ratiba ya utoaji wa vipindi kwenye vyombo vya habari sambamba na utoaji elimu mashuleni na vyuoni.



Akizungumzia suala la mimba/ndoa za utotoni na Ukatili wa Kijinsia amesisitiza umuhimu wa  Kamati za Ulinzi na Usalama za  Halmashauri/Wilaya 

kujadili masuala hayo na kuweka mikakati ya namna ya kuondoa au kupunguza matukio hayo kwenye Jamii.


Alisema  kwamba masuala ya ukatili kwa watoto, mimba/ndoa za utotoni ni suala mtambuka si la kuwaachia Maafisa Ustawi wa Jamii pekee, kwa kuwa Maafisa wa kada hiyo ni wachache ukilinganisha na matukio hayo yanayojitokeza kila kukicha hivyo nguvu za pamoja zinahitajika.


“Natoa wito kwa Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi, kuwahimiza Maafisa Ustawi wa Jamii  kuwapatia takwimu za matukio hayo ili ziweze kujadiliwa katika vikao vya WDC, CMT, CHMT na  Kamati za Ulinzi na Usalama ili kuweka mpango mkakati wa kupunguza matukio hayo kwenye jamii" alisema Jesca.


Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt.Kusirye Ukio  amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii  kufanya kazi kwa juhudi na maarifa huku wakijijengea tabia ya kutathmini kazi zao kwa mujibu wa maelekezo yanayotolewa na  serikali sambamba na kuwahimiza Waganga Wakuu wa wilaya kufanya ufuatiliaji wa  fedha zilizotengwa kutumika kwa wakati kwa ajili ya kutekeleza majukumu yaliyo chini ya kada hiyo.


Naye Meneja wa Mradi wa Kizazi kipya Kanda ya Kati  Shirika la PACT Merina Shaidi alisema  lengo la mradi huo ni kutoa huduma kwa watoto waliothiriwa na walioathirika na Virus Vya Ukimwi – VVU, kutoa huduma za Afya, Elimu, lishe, uchumi, ulinzi na usalama kwa mtoto.


Meneja wa Shirika hilo . Merina amewataka Maafisa ustawi wa Jamii wakati wanapoelekea mwisho wa mradia huo kuendeleza kazi ambazo zimekuwa zikitekelezwa na mradi huo ili kuhakikisha taarifa za ustawi zilizopo kwenye kata zinahifadhiwa kwa usiri mkubwa ili ziweze kutumika wakati zitakapohitajika kama mwongozo  wa Serikali unavyoelekeza.


MWISHO

Share To:

msumbanews

Post A Comment: