Na. Angela Msimbira DODOMA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu ameaagiza Makatibu Tawala Wasaidizi na   wachumi wa Sehemu za Mipango na Uratibu katika Sekretarieti za Mikoa nchini kuhakikisha wanapitia, kuchambua na kutoa ushauri kwenye mipango ya bajeti za maendeleo za Mamlaka za Serikali za Mitaa.


Akiongea na viongozi hao   leo Jijini Dodoma Waziri Ummy amesema jukumu la Makatibu Tawala wasaidizi  na wachumi  ni kuhakikisha wanapitia na kuchambua kwa umakini mkubwa Mipango ya bajeti za maendeleo zinazoletolewa  na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuangalia vipaombele vya Serikali katika kutatua kero za wananchi.


“Kazi yenu si ya kukusanya taarifa za bajeti zinazoandaliwa na  Mamlaka za Serikali za Mitaa pekee, bali mnawajibu wa kuzichachambua kwa weledi  kwa kungalia vipaombele vya Serikali vya kutatua changamoto za wananchi katika sekta ya elimu, afya, barabara na mikopo ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu,” amesisitiza Waziri Ummy


Waziri Ummy amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha fedha zinazokusanywa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo inatatua changamoto za wananchi.


Amewaagiza kuhakikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatenga fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ambapo Halmashauri zinazokusanya zaidi ya shilingi Bilioni 50 zinatakiwa kutenga asilimia 60 ya fedha hizo kwa miradi ya Maendeleo wakati Halmashauri zinazokusanya chini ya bilioni 50 zinatakiwa kutenga asilimia 40.


Amesema kuwa serikali inataka kuona Halmashauri zote nchini zinatenga fedha  za mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa  ujenzi wa vituo vya afya, zahanati,ununuzi wa vitendanishi na dawa, ujenzi wa  madarasa, ununuzi wa madawati, ujenzi wa mabweni, hivyo ni jukumu la makatibu tawala hao kuhakikisha mipango hiyo inaingizwa kwenye Mipango ya bajeti za Mamlaka za Serikali za Mitaa.


“Unapitishaje Bajeti ya Halmashauri wakati haina bajeti ya ujenzi wa madarasa, ununuzi wa dawa na vitendanishi, ujenzi wa shule, mabweni na madawati, hii haikubaliki kasimamieni na kuhakikisha bajeti hizo zinakidhi mahitaji ya wananchi.” amesema Ummy.


Waziry Ummy amewasisitiza Makatibu Tawala Wasaidizi wote nchini kuhakikisha wanasimamia utengaji wa fedha za kuwawezesha wananchi kiuchumi ikiwemo mikopo  wanawake, vijana na watu wenye ulemavu  ili ikalete tija kwa jamii, pia amewataka kuhakikisha fedha hizo zinatolewa kwenye vikundi ambavyo vinaleta tija katika jamii ili kuongeza tija kwa maeneo husika na kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa kwa wakati. 


Aidha Waziri Ummy awataka Makatibu Tawala wasaidizi na wachumi sehemu ya Mipango na Uratibu kuhakikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatenga bajeti kwa ajili ya uendelezaji wa  miji na vijiji kwa kwa maendeleo hayatapatikana  kama hatutawekeza katika uendelezaji miji na vijiji nchini

Share To:

msumbanews

Post A Comment: