Na. Catherine Sungura, Kigoma


Imeelezwa kuwa lengo la Serikali kupitia Mpango wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTD) ni kuhakikisha jamii yote ya watanzania wanaondokana  na athari za magonjwa hayo ifikapo mwaka 2030 ambapo kwa Tanzania kampeni ya kudhibiti magonjwa hayo ilianza mwaka 2009.


Mratibu wa Taifa wa Mpango huo kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt, George Kabona aliyasema hayo jana wakati wa kikao kazi cha uraghibishaji na uhamasishaji kwa viongozi wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri za Mkoa wa kigoma.


Aliongeza kuwa kati ya magonjwa 13 ambayo Mpango huo wanapambana nayo,magonjwa matano   ikiwemo Usubi, Trakoma, Matende na Mabusha, Kichocho na Minyoo ya Tumbo yamepewa kipaumbele katika utekelezaji wa shughuli za kuyadhibiti hivyo yanatakiwa kudhibitiwa mapema kwa njia ya  kugawa kingatiba ngazi ya  jamii pamoja na kwa watoto mashuleni.


“Kwa kupitia takwimu zilizopo Shirika la Afya duniani(WHO) liligundua kwamba magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele yameathiri sana jamii kwa kiasi kikubwa na takribani watu wapatao bilioni 2 walikuwa kwenye hatari ya kupata madhara ya magonjwa haya na hatimaye  kuishi  maisha ambayo watashindwa kuzalisha mali na kuwa mzigo kwa jamii hivyo likaja na  mpango mkakati wa kupambana na kudhibiti magonjwa hayo”.


Dkt. Kabona  pia alitaja mafanikio yaliyopatikana kupitia mpango huo kuwa ni pamoja na  ugawaji wa kingatiba kwa asilimia 100 kwa magonjwa yote matano katika maeneo yote nchini.


 “Kwa upande wa Matende na Mabusha kati ya  Halmashauri 119 zilizokuwa zimeathirika hadi kufikia mwaka huu ni Halmshauri 7 tu ndio bado  zimebaki na  tatizo hilo na kama Wizara  wanaimarisha mkakati wa kumaliza kabisa tatizo hilo”aliongeza Dkt Kabona.


Aidha kwa upande wa ugonjwa wa Trakoma (Vikope) alisema Halmashauri 71 ziliathirika bapo hadi sasa Halmashauri 6 pekee ndizo zimebaki huku na kusema kati ya hizo ni Halmashauri mbili  za Kongwa na Chamwino ugonjwa umerudi baada ya kufaulu kupunguza maambukizi  miaka miwili iliyopita.


"Kufuatia kurudi huko kwa ugonjwa  tunaendelea kufuatilia sababu zake kwa kufanya tafiti za kiutendaji na taarifa itatolewa hivi karibuni"alibainisha.


Aliwataka wananchi kujenga tabia ya kufanya usafi wa uso  ,matumizi wa vyoo pamoja na usafi wa mazingira kwa dhumuni la kuzuia mazalia ya inzi  ili kuweza kujikinga na ugonjwa wa Trakoma.


Kwa upande wa Ugonjwa wa Kichocho na minyoo ya tumbo alieleza kuwa umeathiri Halmashauri zote 184 kwa kiwango tofauti tofauti na kusema  kuwa zipo athari za magonjwa hayo ambazo husababisha utegemezi kwa jamii na kusababisha ndugu wa karibu kushindwa kuzalisha mali kwa sababu ya kutumia muda mwingi na rasilimali kuwahudumia wagonjwa wao.


"Toka mwaka 2008 Mpango umeweza kutoa huduma ya upasuaji wa Mabusha kwa wagonjwa zaidi ya 6000 na huduma hiyo bado inahitajika kwa kiwango kikubwa hasa katika mikoa na Halmashauri za ukanda wa Pwani

kwa ajili ya kuzuia mazalia ya Inzi na hatimaye kutokomeza kabisa magonjwa haya"aliongeza kusema Dkt Kabona.


 Awali akifungua kikao kazi hicho Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ambaye ni Katibu Tawala wa mkoani humo Bw,Rashid Mchatta aliesema Halmashauri zote zinatakiwa kufikia malengo ya asilimia 80 ya umezeshaji kingatiba hizo na kuwataka viongozi wote kushirikiana kwa kubadilishana mawazo ya namna ya kutatua changamoto zilizopo ili kila mmoja aweze kuwafikia watoto wote waliolengwa  kwa kutoa elimu kwa jamii na kuhamasisha wazazi na walezi.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: