Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina akichangia hotuba ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2021/2022 bungeni Dodoma ambapo ameshauri Serikali kuchukua hatua kusaidia wakulima.



MBUNGE wa Kisesa, Mhe.  Luhaga Mpina ameibua bungeni tatizo kubwa  linalochangia kuua viwanda na ajira za vijana wa kitanzania kupitia Kilimo kutokana na mfumo wa kikodi kuwapendelea waagizaji bidhaa kutoka nje ya nchi na kuwakandamiza wazalishaji wa ndani wanaotegemewa kutoa ajira na kukuza uchumi wa nchi.

Hivyo ameshauri Serikali kuchukua hatua ili kumaliza mkwamo huo uliodumu kwa zaidi ya miaka sasa na kuwezesha sekta ya kilimo kukua zaidi kwa kuwezesha wakulima kupata bei nzuri ya mazao yao pamoja na soko la uhakika.

Tunakubaliana kwamba sekta za kilimo, mifugo na uvuvi  ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa letu kwani zinatoa asilimia 25 ya fedha za kigeni,   asilimia 30 ya pato la taifa, asilimia 65 ya malighafi, asilimia 70 ya ajira zote na asilimia 100 ya mahitaji ya chakula ni sekta muhimu na ndio maana tunasema ni uti wa mgongo.

Tanzania inazalisha mazao mbalimbali ambayo mengi yanatumika nchini na mengine yanauzwa nje ya nchi kama tumbaku, korosho, mkonge, michikichi, kokoa, pamba, kahawa, chai, maharage, maharage ya soya, alizeti, maua, matunda, mbogamboga, choroko, mbaazi, ufuta, dengu, viungo, miwa, viazi, mihogo, mahindi, mtama, karanga.

Pamoja na uzalisha huo mpaka sasa kwa takwimu zilizopo tunaagiza chakula kutoka nje ya nchi chenye thamani ya wastani wa sh. Trilioni 1.3 kwa mwaka jambo ambalo ni aibu kwa nchi yetu yenye ardhi nzuri yenye rutuba na fursa lukuki za kilimo. 

Aidha ifahamike pia kuwa zaidi ya asilimia 40 ya watanzania kipato chao kinatokana na kilimo cha zao la Pamba.

Zaidi ya asilimia 40 ya watanzania wote wanategemea kipato chao kupitia zao la pamba.

Takwimu zinaonesha kuwa uzalishaji wetu wa mazao unashuka na mauzo yetu nje ya nchi yanashuka mfano kupitia hotuba ya Waziri uzalishaji wa pamba umeshuka kutoka tani 348,958 mwaka 2019/2020 hadi tani 122,833 mwaka 2020/2021, uzalishaji wa korosho ulishuka kutoka tani 232,631 mwaka 2019/2020 hadi kufikia tani 206,718.88 mwaka 2020/2021.

Waziri anakiri kwamba moja ya sababu za kushuka uzalishaji wa mazao ni kushuka kwa bei na baadhi ya wakulima kuamua kuachana na kilimo. Kama Bunge ni lazima tutafute suluhisho la suala hili.

Hata hivyo kabla sijaendelea na mchango wangu niwapongeza TAHA chini ya C.E.O wao Dk. Jacqueline Mkindi kwa kufanya vizuri sana katika kilimo na biashara ya mazao ya  mbogamboga, matunda, maua na viungo ambapo mauzo yake nje ya nchi yamekuwa yakiongezeka kwa kasi kubwa kutoka Dola za Marekani milioni 412 mwaka 2015 hadi kufikia Dola za Marekeni milioni 779 mwaka 2019.

Tunapozungumzia uzalishaji lazima tujiulize maswali mengi, mwenendo wa uzalishaji wetu wa mazao mbalimbali ukoje, hali ya wakulima wetu ikoje?, hali ya bei na masoko ndani na nje ya nchi ya mazao yao ikoje? 

Serikali inasaidiaje kuongeza uzalishaji wa mazao nchini? changamoto zilizopo za wakulima na wadau wa kilimo zinatatuliwaje, mipango na bajeti tunazoidhinisha zinawagusa vipi wadau wa sekta?

Kwa kifupi sekta ya kilimo inakabiliwa na mizigo mizito ya changamoto kama ifuatavyo 

(i) Upungufu mkubwa wa wataalamu wa ugani, katika maeneo ya kilimo hakuna wataalamu wa kilimo na hivyo wakulima walio wengi hawana wa kuwaelekeza mbinu bora za kilimo, magonjwa ya mimea na matumizi sahihi ya viuatilifu wanalima wenyewe hawana wa kumsaidia.

Mfano katika Jimbo la Kisesa kuna maafisa ugani 15 tu kati ya vijiji 50 na Wilaya ya Meatu kwa ujumla ina maafisa ugani vijijini 33 tu kati ya vijiji 109 tu na kwa hotuba ya Mhe. Waziri anakiri kuwa maafisa ugani waliopo ni 6, 704 wakati mahitaji ni 20,528 kwa takwimu hizi ni wazi kuwa zaidi ya vijiji 7,000 havina afisa ugani hapa nchini.

Kwa nini Serikali imeruhusu upungufu huu uwepo?, huku tunasema kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu lakini hatuwekezi vya kutosha, ni nani anayesaidia wakulima wetu kupambana na magonjwa ya mazao yao?

Ni nani anayesaidia kuongeza uzalishaji mashambani?, nauliza maswali haya muhimu kwa kuwa hata maafisa ugani waliopo hivi sasa wako kama picha tu kwa kuwa hawana usafiri wala posho ya kuwawezesha kuyafikia mashamba ya wakulima.

Kwanini Serikali isiamue leo hii kuajiri maafisa ugani kila kijiji ili kuongeza tija katika kilimo?. Kwa nini Serikali isigawe pikipiki  na posho ya kila mwezi kwa maafisa ugani ili kuwawezesha kuwafikia wakulima? 

Nimpongeze sana Mhe. Waziri kwa kuamua kupeleka pikipiki 1,500 kwa Mikoa ya Dodoma, Singida na  Simiyu na bila kusahau maafisa ugani wa Jimbo langu la Kisesa ambao wanafanya kazi kubwa ya kujituma na wamejitolea kwa muda mrefu hivyo kwa mgao huu ni haki yao kupata pikipiki wote.

(ii) Upatikanaji wa mbegu bora, Waziri ameeleza uzalishaji wa mbegu nchini ambapo amekiri kuwa uzalishaji ni mdogo na sehemu kubwa tunategemea mbegu kutoka nje ya nchi. Kwanini taifa letu hadi leo liendelee kutegemea mbegu za kutoka nje?. 

Inawezekanaje  Taifa ambalo zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wake wanategemea kilimo alafu litegemee mbegu za kuagiza kutoka nje ya nchi?.

Ni kwanini hata mbegu zinazozalishwa hapa nchini zinauzwa kwa gharama kubwa kiasi cha wakulima kushindwa kumudu gharama hizo na kuamua kutumia mbegu za asili ambazo hazina tija, Mbaya zaidi hata taasisi zetu za Serikali zinazozalisha mbegu nazo zinauza mbegu kwa gharama kubwa sana.

Mfano kilo moja ya mbegu ya mahindi na mtama inauzwa kati ya sh. 6,500 mpaka 7,000 wakati kilo ya mahindi inauzwa kwa sh 300 mpaka 500, ni nini kinachosabisha mbegu hizi kuuzwa kwa gharama kubwa kiasi hicho?.

(iii) Mazao mengi ya wakulima yanakabiliwa na magonjwa mfano zao la pamba na mahindi, kumekuwepo wadudu sugu ambao hawafi hata baada ya kupuliziwa viuatilifu/dawa hali inayopelekea hasara kubwa kwa wakulima wetu. Baadhi ya viuatilifu vinavyoingizwa nchini kutoka nje havina uwezo wa kuua wadudu hali inayopelekea hasara kubwa kwa wakulima wetu na taifa kwa ujumla.

Taasisi zetu za utafiti zinafanya nini hadi tuwe na wadudu wasioweza kudhibitiwa? Nani anawafidia wakulima hawa ambao kuingia gharama kubwa ya kununua viuatilifu na baadae mazao yao kushambuliwa na kukosa mavuno?.

Waziri anakiri kuwa TPRI ilipofanya ukaguzi wa kimaabara ukanda wa kusini peke yake yalipatikana maduka 15 yanayouza viuatilifu ambavyo havijasajiliwa, Inawezekanaje hali hii kutokea usimamizi wa TPRI ukoje? Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda na Biashara mko wapi hadi haya yatokee?

(iv) Uanzishwaji wa vyama vya ushirika na kuua soko huria, inawezekana kuna baadhi ya mazao ushirika wa aina hiyo ukahitajika lakini kwa wakulima wa pamba, choroko, ufuta, dengu na alizeti utaratibu huu haufai ni kwanini uanzishe ushirika wa kuwaondoa wanunuzi wengine wote na kubaki wao pekee? Tuelezwe tangu ushirika uanzishwe nchini umesaidiaje upatikanaji wa soko na bei kwa wakulima wa mazao haya?.

Mfumo huu wa manunuzi umeleta changamoto kubwa sana kwa wakulima kwa kushindwa kupata fedha zao kwa wakati kutokana na kukopwa kwa kuwa vyama vya ushirika havina pesa na badala yake wanategemea mpaka wanunuzi binafsi waje kununua katika ushirika wao, wamekuwa wakikusanya pamba au choroko bila kulipia.

Mwananchi mwenye mahitaji ya fedha kwa ajili ya matibabu na ada za wanafunzi atafanyaje? Baadhi ya vyama vya ushirika vimepata hasara na kushindwa kulipa madeni ya wakulima nani anawafidia wakulima hao?

Katika Jimbo langu kuna baadhi ya wakulima wanadai madeni kwa zaidi ya miaka mitatu sasa bila msaada wowote kutokana na pamba kuungua na hasara za vyama vya ushirika, ajira zimekufa mfano katika kijiji kimoja kulikuwa na wanunuzi zaidi ya 10 leo amebaki mmoja hali ambayo imeleta usumbufu mkubwa kwa wananchi kukaa kwenye foleni kusubiri kuuza mazao yao lakini pia ajira za vijana zimekufa.

Waziri anaeleza ushiriki wa vijana katika kilimo na biashara ya kilimo huku wakiwaondoa kwenye mfumo wa biashara kwa kile kinachodaiwa ni ushirika, kwanini tuanzishe ushirika wa kuua soko huria?, kwanini tusiwe na vyama vya ushirika vya kushindana na wanunuzi wengine ili wakulima wachangue na wakauze kwa mwenye bei nzuri. 

Lakini pia ninavyofahamu ushirika unaundwa na wanachama kwanini iwe lazima kwa kila mtu hata hivyo Bunge hili lielezwe ni sheria gani inayowalazimisha wananchi kuuzia mazao yao katika ushirika?

Katika hotuba ya Waziri anathibitisha kuwa vyama vingi vya ushirika havina uwezo na vina changamoto kubwa ya wizi na ubadhirifu wa fedha za ushirika akitolea mfano vyama vikuu vya ushirika 35 vilifanyiwa ukaguzi na COASCO ambapo vyama 17 vilibainika kuwa na wizi na ubadhirifu wa fedha na mali za ushirika.

Vile vile COASCO ilifanya ukaguzi katika vyama vya ushirika 6,021 ambapo vyama vya ushirika 289 tu  vilipata hati safi sawa na asilimia 5 tu huku vyama vya msingi 5,732 vikipata hati mbaya sawa na asilimia 95. Kwa taarifa hizi za ukaguzi wa COASCO kwanini Serikali imeamua kuwahujumu kiasi hiki wakulima wake?

Changamoto kubwa ya wakulima na wadau wa sekta ya kilimo ni ukosefu wa masoko ya uhakika  bei nzuri mazao yao na sababu hii kwa kiasi kikubwa inasababishwa na nchi yetu kuuza mazao kama malighafi katika masoko ya nje.

Hali hii inamepelekea wananchi kuuza mazao yao kwa  bei ya kutupa, kunahamisha ajira na kunufaisha vijana wa mataifa mengine,  watanzania wamegeuka kuwa manamba wa nchi za kigeni kuhaingaika na kilimo wanaonufaika ni nchi za kigeni huku vijana waliowasomesha wenyewe kwa gharama kubwa wakibaki hawana ajira. Kushindwa kukuza uchumi inavyostahili, kushuka kwa mapato ya Serikali na kupungua kwa uwekezaji nchini.

Tanzania inauza malighafi nje ya nchi na kununua bidhaa za viwandani yaani finished product na kusababisha naksi kubwa katika biashara (imbalance of trade).

Kwanini nchi yetu haina viwanda vya kuongeza thamani ya mazao? nini kilichotukwamisha kujenga viwanda vya kuongeza thamani mazao yetu kabla ya kuyauza nje ya nchi? mpaka lini wakulima na wadau na sekta ya kilimo wataendelea kunyonywa kwa kukosa masoko na kupewa bei ndogo?, mpaka lini wananchi wataendelea kuuza malighali katika masoko ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, Agoa, Jumuiya ya Afrika Mashariki, India, China  SADC na nk.

Zipo sababu nyingi zinazotufanya tukose viwanda vya kuongeza thamani mazao nchini kama ifuatavyo:-

(i) Ukosefu wa mitaji ya kujenga viwanda vya kimkakati na hapa ninamanisha viwanda vikubwa vinavyoweza kutoa bidhaa zinazoweza kushindana na bidhaa zingine zozote duniani, baadhi ya wawekezaji wetu wanaotaka kuwekeza kwenye sekta ya kilimo hawana mitaji.

Tutaendelea mpaka lini kusubiri wawekezaji wa kuja kujenga viwanda vikubwa vya nyuzi na nguo zitokanazo na pamba?, tutaendelea mpaka lini kusubiri wawekezaji wakubwa wa kuja kuwekeza viwanda vikubwa vya kubangua korosho yetu yote nchini?,  Tutaendelea mpaka lini kusubiri wawekezaji wa viwanda vikubwa vya kusindika Michikichi, Parachichi, Mpunga, Alizeti, Mahindi nk.

Ushauri wangu kwa Serikali tuanze kutenga fedha kupitia bajeti ya kujenga viwanda vikubwa vya kimkakati ambavyo vitawezesha kuongeza thamani mazao yanayozalishwa na wananchi wetu. Tumeweza kwenye barabara, tumeweza kwenye umeme, hatutashindwa viwanda.

Kwa mfano tunaweza kuanza Kanda ya Ziwa kwa kujenga viwanda vikubwa vitano vinavyotumia malighali ya pamba 1. Kiwanda cha Nyuzi, 2. Kiwanda cha nguo, 3. Kiwanda cha vifaa tiba, 4. Kiwanda cha Mafuta, 5. Kiwanda cha chakula cha mifugo.

Vile Vile ukanda  wa Kusini mwa Tanzania, tutenge fedha za kujenga kiwanda kikubwa cha kubangua korosho na kwa kufanya hivyo kutatuwezesha kutokuuza tena pamba na korosho ghafi nje ya nchi na hivyo kupata soko la uhakika, bei nzuri, ajira, fedha za kigeni  na mapato ya Serikali kuongezeka.

Hapa sisemi kwamba sasa Serikali ifanye biashara isipokuwa kipaumbele cha kwanza ni kuwa na kiwanda chetu suala la nani aendeshe ni uamuzi wetu wenyewe,  tunaweza kukabidhi sekta binafsi iendeshe, tunaweza kuwakopesha watanzania wazalendo kujenga viwanda hivyo kwa masharti nafuu ambayo ni pamoja na kuwadhamini na kuwapa muda mrefu wa kurejesha mkopo huo hata kwa miaka 30.

Kwa kuwa viwanda vinakavyojengwa vitapelekea kuwa na soko la uhakika la  mazao ya kilimo ya watanzania, vitatoa bei nzuri ya mazao na hivyo kuongeza nguvu ya manunuzi (purchasing power) kwa wananchi,  vitalipa kodi za Serikali, vitazalisha ajira za watanzania, vitawezesha kupatikana kwa gharama nafuu bidhaa zinazozalishwa kama nguo.

Jambo la kushangaza pamba inanunuliwa kilo moja sh 1,050, ili kushona shati zinahitajika kilo tatu zenye thamani ya tsh 3,450, shati likishonwa huko China, Indonesia, Thailand, Vietnam na India  na baadae kuuzwa nchini kati ya  sh 50,000 hadi 100,000. TUSIKUBALI HAYA YAENDELEE!

(ii) Mfumo mbaya wa kodi (unsupportive taxation regime) ambapo unakuta kuna baadhi ya kodi zinalinda viwanda vya nje kwa kuweka unafuu wa kodi huku viwanda vya ndani vikitozwa kodi kubwa na kushindwa kushindana,  wawekezaji wetu wamelalamika zaidi ya miaka 10 sasa lakini hakuna muafaka  uliyopatikana na wengine waliokuwa na nia ya kuwekeza waliacha na wengine walifunga viwanda vyao na kufilisika.

Swali la kujiuliza, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara,  Wizara ya Fedha, TRA na Wadau wamefanya tathmini mara ngapi na kubaini kasoro zilizopo katika baadhi ya kodi na hatua gani zilichukuliwa, nimesoma hotuba ya Waziri wa Kilimo sijaona mahali popote amelizungumzia suala hili  jambo hili halijaguswa mahali popote licha ya ukubwa wa tatizo hili ambalo limekuwa machinjio ya uwekezaji nchini.

Tumekuwa na Sera, Sheria na Mipango zinazohamasisha uagizaji wa  bidhaa nje ya nchi badala ya kuzalisha ndani ya nchi yetu, tunahamasisha ujenzi wa viwanda vya nje na kuua viwanda vya ndani. Waziri alihaikishie Bunge hili itakapowasilishwa  Finance bill 2021 itazingatia suala hili.

(iii) Kukosekana kwa ulinzi wa viwanda vya ndani, Leo hakuna ulinzi wa kutosha wa  soko la ndani viwanda vya ndani kunakopelekea ushindani usio wa sawa na wa haki, hivi leo bado kuna uingizaji mkubwa wa bidhaa za kilimo kutoka nje ya nchi ambazo huingizwa nchini bila kulipa kodi, zingine kupitwa na muda wa matumizi, zingine ni feki na bandia zinapoingizwa nchini huuzwa kwa bei ndogo na kuua soko la ndani pamoja na kuua viwanda na ajira nchini.

Mbinu mbalimbali zimekuwa zikitumika ikiwemo kupitia bandari bubu, njia zisizo rasmi, under declaration na under invoice, soko la ndani limevamiwa kwa kuwa hata baadhi ya mazao yanayozalishwa nchini yamekuwa yakiingia kwa wingi kutoka nje ya nchi.

Mfano  maembe, parachichi, nyanya, ma apple, carot hali inayopelekea wakulima wetu kukosa soko wakiteseka kutembea kutwa nzima kutafuta mteja wa fungu moja la maembe nk. mambo haya yanathibitisha ukitembelea kwenye Super Market zetu

Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, TRA,  Vyombo vya Dola mko wapi?

(iv) Kasi ndogo ya Serikali kusaka masoko ya mazao na bidhaa za Kilimo nchini, sioni jitihada za makusudi zinazofanywa na Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano na Kimataifa kupitia Waheshimiwa Mabalozi wote katika nchi mbalimbali wanazotuwakilisha hali hii imepelekea kukosekana kwa masoko na bei nzuri ya mazao ya wananchi.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: