Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Daniel Chongolo akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma leo kwa mara ya Kwanza tangu ateuliwe.
Katibu Mkuu wa CCM,Daniel Chongolo akiteta jambo na Naibu Katibu Mkuu Bara, Christina Mndeme wakati walipofika kuzungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma toka wateuliwe kuongoza Sekratarieti ya Chama hicho.
 Katibu wa NEC,Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka akizungumza katika mkutano wa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo na wandishi wa habari jijini Dodoma leo.



Charles James, 

CHAMA Cha Mapinduzi CCM kimewaonya wale wote waliokua na nia ovu kwenye suala la umeme huku akiitaka Serikali kuwachukulia hatua za kisheria watakaothibitika kuhusika na jambo hilo.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo wakati akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma ambapo ametoa maagizo kwa Serikali kupitia Wizara zake tatu.

Wizara ambazo Katibu Mkuu Chongolo amezitolea maelekezo ni pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Nishati.

Chongolo ameiagiza Serikali kupitia Wizara ya Nishati kuhakikisha inamaliza kwa wakati miradi yote ya Nishati ambayo imeanza kutekelezwa ukiwemo mradi mkubwa wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere uliopo Rufiji mkoani Pwani.

Katibu Mkuu Chongolo amesema kumalizika kwa mradi huo kutaongeza megawati za umeme zipatazo 2115 na kusaidia kuwa na umeme mwingi jambo ambalo litakuza uchumi wa Nchi kupitia viwanda.

" Nionye wale wenye nia ovu na Nchi yetu ambao walitaka kutuweka gizani,niipongeze Serikali kwa hatua za awali walizochukua katika kuhakikisha wananchi wanaepukana na changamoto ya manunuzi ya umeme.

Lakini pia tunaiagiza Serikali kumalizia kuweka umeme vijiji ambavyo vimebaki kwani Ni vichache sana, lengo la Chama chetu ni kuona Nchi nzima inawaka umeme ili kuchochea kasi ya maendeleo kwa Taifa letu," Amesema Chongolo.

Kuhusu Wizara ya Ardhi, Chongolo ameielekeza Wizara hiyo kuongeza kasi yake ya utoaji hati kwa wananchi katika kumiliki ardhi hatua ambayo itasaidia kuwafanya wananchi kuwa na usalama na ardhi yao.

" Tunaelekeza wizara kuongeza kasi kwenye suala la umiliki wa maeneo, CCM kupitia ilani yake ibara ya 74 imeielekeza Serikali kuongeza kasi ya utoaji hati na sisi kama Chama tutalisimamia hili kwa weledi na tunataka kuona Wizara kupitia bajeti yake watueleze wamejipanga kiasi gani kuondoa adha hiyo ya kupoteza ardhi zao kwa kukosa hati.

Kwenye usaminishaji na fidia CCM inaielekeza Serikali kuwalipa wananchi stahiki zao kwa wale wote waliotwaliwa maeneo yao kisheria, na niwaagize viongozi wetu kuanzia ngazi ya Mitaa na Vijiji hadi Wizarani kutatua changamoto za ardhi,"Amesema Chongolo.

Kwenye sekta ya Kilimo, Katibu Mkuu Chongolo ameielekeza Wizara ya Kilimo kukamilisha ujenzi wa skimu katika wilaya ya Songea na Rungwe huku akiitaka Serikali pia kuongeza tija na faida katika uzalishaji.

" Kutokana na kuwa na changamoto ya mbegu Chama kinaielekeza Serikali kuongeza bajeti ya utafiti wa mbegu ili kuwahakikishia wakulima ubora wa mbegu wanazonunua," Amesema Chongolo.


Share To:

msumbanews

Post A Comment: