Katibu wa Asasi ya Mapambano ya Kifua Kikuu na Ukimwi Tanzania (MKUTA) Mkoa wa Singida, Michael Moses (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafunzo yaliyotolewa leo kwa madiwani na wakuu wa idara wa Manispaa ya Singida   juu ya kifua kikuu (TB) na ukimwi kwa watoto. Kushoto ni Mwenyekiti wa Asasi hiyo, Salim Ali na Mratibu wa asasi kwa mikoa ya Tabora na Singida, Sadam Kidera.


Mwenyekiti wa Asasi hiyo, Salim Ali, akizungumza katika mkutano huo.

Mratibu wa asasi hiyo kwa mikoa ya Tabora na Singida, Sadam Kidera.  akizungumza katika mkutano huo.


Na Dotto Mwaibale, Singida


MADIWANI na wakuu wa idara wa Manispaa ya Singida wamepatiwa mafunzo ya siku juu ya kifua kikuu (TB) na ukimwi kwa watoto,kwa ajili ya kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi.

Mafunzo hayo yametolewa na Asasi ya Mapambano ya Kifua Kikuu na Ukimwi Tanzania (MKUTA) kupitia mradi wa CAP TB-Singida kwa ufadhili wa EGPAF unaohusisha mikoa ya Tabora na Singida katika kukabiliana na tatizo la TB na Ukimwi kwa watoto.

Akizungumza jana katika mafunzo hayo Mratibu wa mradi huo wa mikoa hiyo,  Sadam Kidera alisema kuwa bado kuna imani potofu miongoni mwa jamii kwamba mtoto anapougua magonjwa hayo anaonekana kuwa  amerogwa.

Kutokana na hali hiyo alisema  watoto wanapobainika kuugua maradhi hayo ni vema jamii ikachua hatua za kuwapeleka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya badala ya kuamini imani za kishirikina.

"Ni vema na jukumu letu kuwafikishia wananchi na jamii kwa ujumla umuhimu na kutambua kwa kina zaidi kwamba ni suala la muhimu na msingi waweze kuchukua tahadhari  na elimu kutolewa jinsi gani ya kupata matibabu." alisema Kidera.

Aidha Kidera alibainisha kwamba magonjwa hayo ni hatari, hivyo ni vema jamii ikachukua hatua ya kukabiliana nayo mapema  kwa kuwa yanatibika.

Katibu wa Mkuta Mkoa wa Singida,  Michael Moses alisema kuwa jamii inapoona dalili za watoto wao kuugua Kifua Kikuu na Ukimwi inapaswa kuwapeleka mara moja kwenye vituo vya kutolea tiba, tayari kwa ajili ya kupatiwa matibabu sahihi.

Mradi huo unaotekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja mkoani Singida kuanzia Juni,  2020 na kufikia tamati juni mwaka huu utaiwezesha jamii kuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na magonjwa hayo. 

Share To:

Post A Comment: