Shekh wa Mkoa wa Rukwa kutoka Baraza kuu la Waislamu Tanzania Shekh Rashid Akilimali akitoa nasaha zake kabla ya kusoma dua maalum ya Kumuombea Hayati Dkt. John Pombe Magufuli  Askofu Ambele Mwaipopo wa Kanila la KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika Rukwa na Katavi akitoa nasaha zake fupi kabla ya kuanza kwa dua.  Mhasham Baba Askofu Beatus Urasa wa Kanisa Katoliki jimbo la Sumbwanga akiomba dua mbele ya wananchi waliohudhuria katika dua hiyo maalum iliyoongozwa na kamati ya Amani Mkoa wa Rukwa .

 Baadhi ya wananchi waliohudhuria kwenye Dua maalum ya Kumuombea aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika viwanja vya Kumbukumbu ya Nelson Mandela mjini Sumbawanga.



Viongozi wa Dini Mkoani Rukwa wakiongozwa na Kamati ya Amani Mkoani humo wameendesha dua maalum ya kumuombea aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyeaga dunia tarehe 17.3.2021.

Dua hiyo maalum iliyofanyika katika viwanja vya Kumbukumbu ya Nelson Mandela Mjini Sumbawanga ilihudhuriwa na wananchi mbalimbali wakiwemo, wazee maarufu, wazee wa kimila, watumishi wa sekta mbalimbali Pamoja na wamachinga.

Awali, Kabla ya kuanza kwa dua hiyo, Mwakilishi wa mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Karolius Misungwi alitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya tano chini ya aliyekuwa Rais wa awamu hiyo Hayati Dkt. John Pombe Magufuli Pamoja na kumpongeza Rais wa awamu ya Sita Mh. Samia Suluhu Hassan na kumtakia utekelezaji mwema wa majukumu yake.

“Nichukue Fursa hii kwa niaba ya mkuu wa mkoa wetu kumpongeza sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa na kuwa rais wetu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwenyezi Mungu amuongoze katika kuwatumikia watanzania wote bila ya kujali itikadi zao, bila ya kujali rangi zao, na bila ya kujali makabila yao”.

“Sisi hatuna mashaka kabisa na umahiri wa rais wetu mpendwa Mh. Samia Suluhu Hassan kwakuwa tunajua kuwa atayaendeleza yote yale aliyoyaacha aliyekuwa mtangulizi wake, kazi tuliyonayo sisi wanarukwa ni kumuombea na kumpa ushirikiano katika kulijenga taifa letu,” Alisema.

Aidha, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Amani Baba Askofu Ambele Mwaipopo wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika Rukwa na Katavi alieleza Ushujaa wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli juu ya namna alivyoweza kupigania maslahi ya watanzania na hasa wanyonge.

“sisi wanarukwa, kutoka dini na madhehebu yetu yote,tumekutana mahali hapa katika umoja wetu, ili kwa Pamoja tuutafute uso wa Mungu ili katika msiba huu Mungu Mwenyezi atujaalie ustahimilivu akiachilia amani na mshikamano miongoni mwetu, tunamuomba Mungu Taifa letu liwe na mshikamano, amani kati yetu watanzania itamalaki licha ya msiba huu mkubwa wa kuondoka kwa aliyekuwa rais wetu wa awamu ya tano Dkt. Magufuli,” Alielezea.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Rukwa Shekh Rashid Akilimali baada ya kuelezea kazi nzuri iliyofanywa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alimuombea Rais Mh. Samia Suluhu Hassan aweze kuvivaa viatu vilivyoachwa na hayati magufuli ikiwa ni Pamoja na kuwashughulikia wezi na wala rushwa ndani ya serikali.

“Tunamuombea avae viatu hivyo, awe madhubuti na imara, akaze Kamba ile ile, madhalimu, majizi ndani ya serikali, wala rushwa nidhamu maofisini irudi kama ilivyokuwa kwa Rais Magufuli, tunaona nidhamu ilikuwepo, ulikuwa ukienda maofisini unaulizwa si miaka ya nyuma na lile neno la pili unaniachaje halikuwepo tena, na walichukia sana madhalimu na wezi ndani ya serikali,” Alisema.

Dua hiyo maalum imefanyika ikiwa ni kuungana na watanzania wote nchini kumuombea aliyekuwa Rais wa Taznania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ili Mwenyezimu Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi.
Share To:

Post A Comment: