Msimamizi  wa Ujenzi wa Bwawa la Kunyweshea Mifugo la Chamakweza, Robert Baltazar akimuonesha michoro ya bwawa hilo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (wa kwanza kulia) alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa bwawa hilo lililopo Chalinze, Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani Februari 24, 2021. Wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi, Evarist Ndikilo.

      Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul akijadiliana jambo na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo (kushoto) na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (kulia) alipofanya ziara kukagua Kituo cha Ukaguzi wa Mifugo cha Ruvu Darajani kilichopo Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani jana.
      Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Rogers Shengoto akijibu moja ya hoja ziliyoibuliwa katika ziara ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul aliyoifanya Mkoani Pwani. 

       


      Na Mbaraka Kambona, Pwani

       

      Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amemsimamisha kazi Mkuu wa Kituo cha Ukaguzi wa Mifugo cha Ruvu Darajani, Gabriel Lyakurwa kwa tuhuma za kutorosha mifugo na kusababisha upotevu wa mapato ya Serikali, huku akimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi, Evarist Ndikilo kuwachukulia hatua Watumishi waliochini ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ambao walikuwa wanashirikiana na Mkuu huyo wa kituo.   

      Gekul alitoa maamuzi hayo baada ya Mkuu huyo wa Mkoa wa Pwani kuibua tuhuma hizo katika ziara yake aliyoifanya kwenye kituo hicho kilichopo Ruvu Darajani, Wilayani Bagamoyo jana. 

      Mhandisi Ndikilo alisema uchunguzi alioufanya umebaini kuwa Mkuu wa kituo hicho amekuwa akishirikiana na wenzake wasiowaaminifu kutorosha mifugo inayopelekwa katika kituo hicho kwa ajili ya kukaguliwa kabla ya kuruhusiwa kupelekwa katika maeneo mengine ya minada. 

      “Mhe. Naibu Waziri nimefanya uchunguzi wa kina na kugundua kuwa utoroshaji huu unahusisha mtandao wa watu wengi wakiwemo baadhi ya Wananchi, Wafanyabiashara na Watumishi wa Serikali…, kwa mfano tarehe 17 mwezi huu wa pili kuna Magari matano yalileta ng’ombe katika kituo hiki kwa ajili ya kukaguliwa lakini ni gari moja tu lililokwenda Dar es Salaam kama kawaida ilivyo, huku mengine yaliyobaki yakichepushwa na mifugo ilipelekwa Kisarawe, Kibaha na Kijiji cha Kidogozero kinyemela,” alisema Mhandisi Ndikilo. 

      Kufuatia tuhuma hizo, Naibu Waziri Gekul alitoa maagizo hayo ya kusimamishwa kazi mkuu huyo wa kituo huku akisema kuwa Wizara itaunda tume maalum kwa ajili ya kwenda kuchunguza tuhuma hizo ikiwemo kupitia mahesabu yote ili kubaini ni kwa kiasi gani mapato ya Serikali yamepotea na wale wote watakaoonekana kuhusika katika upotevu huo watachukuliwa hatua kali. 

      "Hatuwezi kucheza na maduhuli ya Serikali, haiwezekani tuwe na ng’ombe zaidi ya milioni 33 lakini mchango wa sekta ya mifugo katika pato la taifa hauzidi asilimia 7, ni kwa sababu ya michezo kama hii, hatutakubali, na tutakwenda kukagua katika maeneo yote ya minada," alisema Gekul. 

      Naye, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete alisema kuwa katika jambo ambalo wamekuwa wakilisemea sana ni kituo hicho kukithiri kwa vitendo vya ubadhilifu ambavyo vimekuwa vikichangia Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kupoteza mapato. 

      Ridhiwani alimuomba Naibu Waziri huyo kuhakikisha anachukua hatua madhubuti za kudhibiti vitendo hivyo vya ubadhirifu ikiwemo kuondoa mtandao wote wa waharifu ili halmashauri iweze kupata mapato yanayostahili.

      Share To:

      Post A Comment: