Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza katika ofisi ya Mkuu wa  wa Lindi tarehe 5 Januari 2021 wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya Ardhi na uhamasishaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi. Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Lindi Godfrey Zambi na kulia ni Afisa Tawala wa Wizara ya Ardhi Baraka Mraha.  

Na Munir Shemweta, WANMM LINDI


Katika kinachoonekana kusogeza huduma za Mabaraza ya Ardhi na Nyumba katika wilaya mbalimbali nchini, Serikali imewaelekeza Makatibu Tawala wa mikoa kuhakikisha wajumbe Washauri wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba wanateuliwa kwa ajili ya kuhudumia wilaya zisizokuwa na Mabaraza ili kuondoa kero kwa wananchi  kutembea umbali mrefu kuzifuata huduma hizo.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula tarehe 5 Januari 2021 mkoani Lindi wakati akizungunza na Watendaji wa Sekta ya Ardhi, uongozi wa mkoa wa Lindi na Wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo akiwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serilali kupitia kodi ya pango la ardhi.

Maelezo ya Dkt Mabula yanafuatia kuelezwa na Mkuu wa mkoa wa Lindi Godfrey Zambi kuwa mkoa wake una Baraza moja la Ardhi na Nyumba linalohudumia wilaya zote tano za mkoa huo jambo alilolieleza kuwa limekuwa likileta usumbufu na kero kwa wananchi kutembea umbali mrefu.

" Mkoa wetu una Baraza moja tu la Ardhi na Nyumba la wilaya linalohudumia wilaya za mkoa huu, fikiria mtu anatoka Liwale kuja hapa umbali wa kilometa 250  au Kilwa Kimeta 200 ni kumuumiza mwananchi" Alisema Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi.

Kwa sasa kuna jumla ya Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya 57 yanayotoa huduma nchini wakati sheria inataka kuwa na Mabaraza 139 jambo linalosababisha baadhi ya wilaya kukosa huduma za Mabaraza na kuwafanya wananchi kuzifuata  huduma kwa kutembea umbali mrefu.

Dkt Mabula alisema, baada ya Serikali kuona wananchi wanapata shida ya kuzipata huduma za Mabaraza ya ardhi sasa imeamua kuwaelekeza Makatibu Tawala wa Mikoa kuteua  wajumbe Washauri wa Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya sambamba na  Wakurugenzi wa Halmashauri kutakiwa kutenga ofisi itakayoendesha Mashauri na kuwa na Watumishi kama Makarani ili kuwawezesha Wenyeviti kufanya kazi  kulingana na mahitaji ya wilaya husika.

"Pamoja na kuwa na Mabaraza ya Ardhi katika wilaya mbalimbali lakini tumeona bado kuna 'gape' mahali hasa zile wilaya ambazo hazina Mabaraza ya Wilaya, maana Baraza la wilaya moja linahudunia wilaya tatu kwa hiyo bado hatujatatua tatizo la wananchi kusafiri umbali mrefu ili kusogeza huduma kwa wananchi wanaoteseka" Alisema Dkt Mabula.

Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya kwa mujibu wa sheria Na 2 ya mwaka 2002 lina wajumbe wasiozidi saba na watatu kati yao ni wanawake na kuteuliwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na Mapendekezo ya Mkuu wa Mkoa kutoka katika eneo la wilaya husika.


Share To:

Post A Comment: