SINGIDA


Naibu waziri wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI Mhe. David Silinde amemvua madaraka mkuu wa shule ya Lulumba Halmashauri  ya Wilaya ya Iramba na kuagiza afisa elimu sekondari kuandika maelezo ya kwanini jengo la bweni halijakamilika kwa  wakati huku fedha zikiwa zimepelekwa toka mwezi wa sita mwaka 2020 na ikitakiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu.


Pia Naibu Waziri Silinde amevunja kamati ya ujenzi ya shule hiyo kwakushindwa kusimamia.


Hatua hiyo ameichukua baada ya kufanya ukaguzi wa fedha za mradi wa lipa kulingana na matokeo (EP4R) kwa kuboresha utoaji wa elimu nchini.


Wakati huo huo Mhe. Silinde ameagiza ujenzi wa bweni hilo ukamilike ifikapo mwisho wa mwezi Januari kwa kiasi cha fedha zilizoletwa na Serikali ambazo shilingi milion 80 badala ya gharama alizotoa mkuu wa shule hiyo milion 146 na kutolea mfano wa wilaya ya ikungi ambao wamekamilisha  bweni la aina hiyo kwa gharama ya shilingi milion 80.


Kwa upande wake mkuu shule ya Lulumba Jeremia Kitiku  alidai kilichochelewesha ujenzi huo ni kupanda kwa bei ya cement na wananchi kutoshiriki kikamilifu hivyo kuongeza gharama za ujenzi.


Katika shule ya msingi ya Ntwike katika Wilaya hiyo Naibu waziri Silinde amemtaka afisa elimu msingi wa wilaya ya iramba kuandika barua ya kwanini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kushindwa kukamilisha ujenzi wa madarasa manne yenye thamani ya shilingi milioni 80 huku fedha zikiwa zimefika shuleni hapo miezi sita iliyopita.

Share To:

Post A Comment: