Na Tito Mselem, Dodoma

Dhana ya Serikali kufanya mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 ni kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini kuchimba kwa tija na kuzalisha kwa faida.


Kauli hiyo, ameitoa Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya alipotembelea Mgodi wa Handali uliopo Wilaya ya Chamwino jijini Dodoma ambapo alizungumza na kutatua kero za wachimbaji wadogo katika Mgodi huo.


Imeelezwa kuwa Mgodi wa Handali ulianza miezi sita iliyopita na ulianza kama mlipuko wa madini ya dhahabu (Rush), ambapo mpaka sasa una mialo 28 kalasha 30 na umeweza kuvuna dhahabu ya Uzito wa Gramu 816.77 yenye thamani ya Shilingi 89,293,000/- na dhahabu inayopatikana eneo hilo ina kiwango cha ubora cha asilimia 80.


Aidha, Prof. Manya amesema, Shughuli za madini zimeimarishwa ambapo kila Mkoa kuna Afisa Madini Mkazi ambaye yupo eneo husika kwa ajili ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini wa Mkoa husika.


“Niwaombe wachimbaji wadogo wa madini kote nchini kuzitumia Ofisi za Maofisa Madini Wakazi katika maeneo yenu ili wawape ufafanuzi wa changamoto yoyote katika maeneo yenu na myatumie Masoko ya Madini yaliopo sehemu mbalimbali nchini kuuzia na kununulia madini yenu na kwa yoyote atakaye kiuka atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufilisiwa, faini, kwenda jela, au kufutiwa leseni na kuzuiliwa kujihusiha na shughuli yoyote inayohusiana na Madini,”   alisema Prof Manya.


Pia, Prof. Manya amewataka wachimbaji wadogo wa madini nchini kupendana, kushirikiana, kuthaminiana na kuachana na wivu, fitina na majungu ili wafanye shughuli zao kwa tija ambapo mpaka sasa Serikali imewawekea mazingira wezeshi wachimbaji wadogo na kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara ya Madini na Mikoa, Wilaya mpaka kwenye ngazi ya Vijiji katika shughuli za madini.


Vile vile, Prof Manya amemuagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma Nchangwa Marwa kutoa elimu ya Uchimbaji Salama kwa wachimbaji wadogo katika mgodi huo, ambapo alisema hayo kutokana na mvua za masika zinazoendelea kunyesha nchini kote.


Katika hatua nyingine, Prof. Manya, amewataka madalali wote wa madini (Brocker) kuhakikisha wanafanya biashara na wawe na leseni za biashara ya madini ambaye hana alielekezwa amuone Afisa Madini Mkazi wa Mkoa huo. 


Naye, Mkuu wa Wilaya Chamwino Vumilia Chamiga alimshukuru Prof. Manya kwa kusikiliza na kuzitatua kero za wachimbaji wadogo wa Mgodi huo na kuahidi kwamba atashirikiana na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma ili watoe elimu ya Uchimbaji Salama hasa katika kipindi hiki cha mvua.

Share To:

Post A Comment: