Friday, 22 January 2021

KIWANDA CHA TWIGA CEMENT WAMKABIDHI RC KUNENGE MIFUKO 800 YA SARUJI KWAAJILI YA UJENZI WA MADARASA DAR.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Aboubakar Kunenge Leo amepokea mchango wa mifuko 800 ya Saruji kutoka Kiwanda Cha Twiga Kama sehemu ya kuunga mkono jitiada za Serikali ya Mkoa huo Katika kutatua changamoto za uhaba wa Vyumba vya madarasa.


Akipokea Mchango huo RC Kunenge amesema Saruji hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa katika Ujenzi wa Vyumba vya madarasa na kuwezesha wanafunzi kusoma pasipo usumbufu wowote.

Aidha RC Kunenge amesema hadi kufikia Sasa Mkoa huo umekamilisha Ujenzi wa Madarasa 80 kati ya madarasa 339 yanayojengwa kwaajili ya wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato Cha Kwanza na kukosa nafasi Kutokana uhaba wa madarasa ambapo ameeleza kuwa Hadi kufikia February 28 madarasa yote yatakuwa yamekamilika.

Hata hivyo RC Kunenge amesema changamoto za uhaba wa Vyumba vya madarasa ni matokeo mazuri ya mwitikio wa wananchi Katika suala la elimu bila malipo ambapo kwa mwaka huu pekee makadirio ni kuandikisha wanafunzi zaidi ya 78,000 wa darasa la Kwanza.

Baada ya kupokea shehena hiyo ya Saruji RC Kunenge amekabidhi kwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo alieambatana na Mkurugenzi wa Manispaa na Meya wa Manispaa hiyo na kuwataka kuhakikisha Saruji hiyo inaenda kufanya kazi iliyokusudiwa.

Kwa upande wake Meneja Biashara wa Kiwanda Cha Twiga Cement Mhandisi Danford Semwenda amesema wameamua kutoa mchango huo Kama sehemu ya utatuzi wa changamoto za elimu kwa jamii ambapo wamemuahidi RC Kunenge kuwa wataendelea kushirikiana na Mkoa kwenye masuala mbalimbali ya kijamii.No comments:

Post a Comment