NA


NAMNYAK KIVUYO,ARUSHA



Naibu waziri ofisi ya waziri Mkuu kazi,vijana ajira na walemavu Ummy Nderiananga amewasisitia wanaosimamia ujenzi wa vyumba vya madarasa kuhakikisha miundombinu inakidhi mahitaji ya walemavu.


Nderiananga aliyasema hayo mkoani Arusha  alipotembelea ujenzi  wa vyumba vya madarasa unaoendelea katika shule mbalimbali  za jiji la Arusha ambapo aliwataka wanaosimamia ujenzi huo kuhakikisha miundombinu rafiki kwa wenye ulemavu inakuwepo katika madarasa hayo.


"Nilikuwa napita kuelekea Dodoma nikaona siyo dhambi kupita hapa kuwatia moyo vijana wenzangu  mnaoendelea kujitolea  kuwajengea wadogo zenu pamoja na watoto wenu mahali pa kupatia elimu yao, serikali inavutiwa sana na kazi mnayoifanya , nitoe rai kwa wasimamizi wa ujenzi hakikisha mnaweka miundombinu rafiki kwa wenye ulemavu ili kuendana  sawa na sera ya usawa," Alisema Nderiananga.


Naye Mkuu wa mkoa wa Arusha  Iddy Kimanta alisema mkoa wa Arusha  kwa wilaya zote sita inakabiliwa na uhaba wa vyumba zaidi ya 100 lakini kabla ya februari yatakuwa yamekamilika kwa asilimia 100.


"Nitumie fursa hii kumhakikishia Waziri Mkuu ambaye alitoa maelekezo ya kujengwa vyumba vya madarasa vya kutosha nchi nzima kuwa sisi mkoa wa Arusha haitafika Feb. 28 bila kukamilika tupo katika hatua mzuri" Alisema Kimanta.


Alisema mkoa mzima zipo Wilaya mbili ambazo hazina upungufu wa madarasa ikiwemo Wilaya ya Karatu pamoja na Longido ambapo aliwashukuru wananchi kuhakikisha madarasa yanakamilika kwa kutoa muda wao kujenga bila malipo.



Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya  Arusha Kennan Kihongosi aliwataka wananchi kuendelea kujitokeza na kujitolea katika ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa lengo la kuepusha uhaba wa madarasa kutokana na ongezeko la wanaojiunga kidato cha kwanza 2021.


“Ninawashukuru wananchi kwa  moyo wa uzalendo mliouonyesha kwa serikali kwa namna mlivyojitoa kuijenga nchi yenu na kumuunga Rais mkono katika juhudi za elimu bure hiyo  nitoe rai endeleeni kujitokeza katika shule zote ambazo ujenzi unaendelea  lakini pia  lindeni rasilimali za serikali hususani miundombinu ya shule,” Alisema Kennan.


Aidha Kihongos alisema wapo baadhi ya watu wanahujumu miundombinu ya shule  kwa maslahi binafsi au kwa kutumwa jambo ambalo alikemea na kuongeza kuwa ni wajibu wa kila mmoja kulinda rasilimali za nchi.


Alimshukuru Mh. Rais kwa kutenga billion 24.5 kila mwezi kwa ajili ya elimu bure ambapo aliahidi kuhakikisha wanasimamia vuzuri maendeleo ya elimu kwa kutoa ushirikiano kwa  ngazi zote husika.



Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt John Pima alisema ipo miradi zaidi ya minne inayotekelezwa katika jiji la Arusha kwa ajili ya Ujenzi wa  vyumba vya madarasa  ikiwemo Shule ya sekondari Muivaro,Elerai,Terati, pamoja na Shule mpya ya Ungalimited inayotarajiwa kuanza kidato cha kwanza 2021.


 Dkt Pima alisema Halmashauri ya jiji la Arusha inakabiliwa na upungufu wa madarasa 16 lakini kwa sasa wanakenga madarasa 36 ili kuweza kujiandaa na miaka mingine zaidi ambapo baadhi ya maeneo wanakaribia kumalizia ujenzi.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: