NA MWANDISHI WETU, CHALINZE.


MBUNGE Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete  amesema muda wa kazi ni sasa, hakuna kulala wala likizo ilikuwatumikia watanzania wanyonge.


Ridhiwani ambaye amekuwa katika shughuli mbalimbali za Kijimbo, ambapo tarehe 27 Desemba 2020 licha ya kuwa ni siku ya mapumziko,  ameweza kufanya ziara ikiwemo kukagua shule za Sekondari zaidi ya 6 pamoja na ukaguzi wa soko la kisasa linalojengwa Bwilingu-Chalinze Mjini.


Awali akikagua soko hilo na kujionea maendeleo yake pia aliweza kuonana na baadhi ya  wafanyabiashara wakiwemo Jumuiya ya wachinjaji kuku na nyama.


"Mkandarasi ametuhakikishia ujenzi unaendelea vizuri na  kwa kasi. Pia nimepata kukagua vizimba vyake katika soko hili ambalo litakuwa kitega uchumi ndani ya Halmashauri yetu.


Soko hili ni moja ya utekelezaji wa ilani ambao unakwenda sio tu kuupa sura mji wa Chalinze lakini unakwenda kubadilisha na maisha ya watumiaji wa soko na njia tunazofanya biashara". Alisema Ridhiwani Kikwete.


Mbali na ukaguzi wa soko hilo, pia Ridhiwani Kikwete amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani na Maagizo ya viongozi kuhusu mustakabali wa Tanzania ya agenda ya Elimu huku akiambatana  na Watendaji wa Idara ya Elimu Sekondari na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze, Ramadhani Possi.


"Tumetembelea shule 6 ikiwemo shule ya sekondari Chalinze, Chahua,Msata, Kiwangwa, Changalikwa, Rupungwi na Mandela wasichana.


"Tumeshuhudia maendeleo makubwa yaliyokwisha fanyika ikiwemo ujenzi  wa madarasa, mabweni na ofisi za walimu" Alisema Ridhiwani Kikwete na kuongeza:


Pamoja na hayo Mbunge ameshuhudia ujenzi wa madarasa 17 unaoendelea katika maeneo mbalimbali yanayotaraji kukamilika kabla ya tarehe 17 ili yawe tayari kutumiwa katika mwaka mpya wa Elimu.


Ziara ya Mbunge inaendelea katika Kata mbalimbali.


Mwisho.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: