Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Singida, Thomas Nyamba akiongea na Waandishi wa Habari.

Mwenyekiti wa   Chama Kikuu Cha Ushirika  cha Wakulima Mkoa wa Singida (SIFACU LTD) Yahaya Ramadhani  akiongea na Waandishi wa Habari

Wajumbe wa Bodi na Watendaji wa   Vyama vya Ushirika  katika  Mkoa Singida  wakipewa  mafunzo.

 

John Mapepele na Rose Nyangasa, Singida

Mkoa wa Singida  umeandaa  mafunzo  ya siku  tatu ya kuwajengea  uwezo Wajumbe wa Bodi na Watendaji wa   Vyama vya Ushirika  katika  Mkoa ili kuwasaidia  kuacha  kufanya kazi kwa  mazoea  badala yake wafanye  kazi  kwa weledi na kwa kuzingatia sheria  huku wakitanguliza mbele maslahi ya wakulima.  

 

Akifungua mafunzo hayo leo mjini Singida kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia eneo la Uchumi Beatus Choaji amesema Mkoa umeamua kufanya  mafunzo hayo kutokana na kupata  taarifa  ya ukaguzi uliofanywa kwenye vyama vya ushirika  kushindwa  kufanya vizuri.

 

Choaji amesema Serikali ya Awamu ya Tano ipo macho kwa viongozi wa Vyama Vya Ushirika na maafisa wengine wa Serikali ambao wamekuwa wakishirikiana  na walanguzi kuwanyonya wakulima ambapo amesema hili ni  kosa kisheria  na  kuwaonya kwamba  katika kipindi cha  sasa Sheria kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuwatia hatiani kwa Sheria ya Uhujumu Uchumi.

 

 “Nawaagiza Watumishi wa Serikali kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake fanyeni kazi kwa weledi na kuzingatia Sheria huku mkitanguliza mbele maslahi ya wakulima”aliongeza  Choaji

 

Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Singida, Thomas Nyamba amesema lengo la  kuandaa mafunzo hayo ni kutoa elimu  ya kuwawezesha Watendaji ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

 

Nyamba amesema kumekuwa na makosa mbambali ya kiuzembe  na kitaaluma katika utendaji wa kazi lakini kupitia mafunzo haya watendaji wote watabadilika.

 

Mwenyekiti wa   Chama Kikuu Cha Ushirika  cha Wakulima Mkoa wa Singida (SIFACU LTD) Yahaya Ramadhani  amesema pamoja na mambo mengine wajumbe wa kikao hicho watafundishwa masomo ya uandishi wa vitabu vya mwanzo na vitabu vikuu,uaandaaji wa taarifa za fedha,uongozi na utawala pia na Sheria ya Vyama Vya Ushirika Na.6. ya Mwaka 2013

 

Ameyataja masomo mengine yatakayo fundishwa kuwa ni uandaaji wamakisio ya mapato na matuminzi,uandaaji wa mpango mkakati, utatuzi wa migogoro na usimamizi wa fedha na udhibiti wa rushwa katika vyama vya ushirika.

 

Baadhi ya washiriki katika wa mafunzo hayo wamepongeza juhudi za Serikali ya awamu ya Tano kutoa mafunzo na kusema kwamba yataongeza tija katika utendaji wao wa kazi.

 

Mwenyekiti wa AMCOS wa Wilaya ya Ikungi Mnang’ana Rukia Jumanne amesema mafunzo hayo yamewasaidia kutambua majukumu ya kila mmoja kwenye vyama vya ushirika hivyo yatawawezesha kufanya kazi bila kuingiliana nakwa weledi tofauti na kipindi cha awali.

 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi amesisitiza kwamba   kwa sasa Serikali  imeweka  mikakati madhubuti ya kuufanya  Mkoa wa Singida  kuwa  miongoni mikoa itakayozalisha kwa  wingi mazao na  kuilisha Tanzania na nchi  mbalimbali za Afrika  na dunia kwa ujumla na hivyo kuwa na  Vyama vya Ushirika  makini ni jambo  lisiloepukika  kwenye Mkoa wa Singida.

“Tumeanza vizuri kwenye zao la Korosho na Alizeti sasa tunaongeza nguvu kufufua na kuanzisha mazao ya Mkonge na Parachichi” aliongeza Mhe. Nchimbi

 

 

 

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: