Mmoja wa wakulima wa zao la Mtama katika eneo la Kibaigwa wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma,Sebastian Msola (Kulia) akitoa maelezo kwa ujumbe kutoka TBL , WFP na FtMA walipofika kumtembelea shambani kwake mwishoni mwa wiki wakati wa tathmini ya mradi wa pamoja wa kuwezesha wakulima wa zao hilo katika mikoa ya Dodoma na Manyara

 

Baadhi ya wakulima wa mtama wanawake katika mkutano wa tathmini


======  =======  =========

Bi Hilda Madeje, mkulima wa mtama katika kijiji cha Sagala B kilichopo wilayani Kongwa mkoani Dodoma.sasa ana soko la uhakika la kuuzia magunia 30 ya mtama ambayo ni ongezeko la 70% kulinganisha na miaka ya nyuma.Hali hii imemuwezesha kupata fedha za kutosha kujenga nyumba ya kuishi familia yake na kulipia ada ya shule kwa watoto wake  4.

Bi Madeje ni mmoja wa washiriki wa mradi wa majaribio wa kilimo cha mtama  wa kampuni ya bia  ya TBL Plc, taasisi ya Farm to Market Alliance(FtMA) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), ambao ulilenga kuwawezesha wakulima wa mtama  mbinu za kisasa za kulima zao hilo kwa kuwapatia mbegu bora za mtama na kuongeza mavuno sambamba na kuwahakikishia soko la uhakika la mavuno yao.

Mradi huu wa ushirikiano ulianza mwezi Januari 2020 ambapo kampuni ya TBL Plc ilikubali kununua mtama unaozalishwa na wakulima mkoani Dodoma, TBL Plc, FtMa na WFP iliwasaidia wakulima hao kupata mbegu ya mtama; bima ya mazao; itifaki za usimamizi wa zao la mtama; huduma za ugani za kilimo; pamoja na ujumuishaji bora na soko la uhakika ili waweze kuongeza mavuno yao.

Akizungumza wakati wa tathmini ya msimu uliopita iliyofanyika mkoani Dodoma wiki iliyopita, Meneja Kilimo wa TBL Plc, Joel Msechu, alisema kuwa TBL Plc ililipa wakulima wadogo jumla ya Tzs 1.75 bilioni kwa ajili ya kununua tani 3,000 za mtama uliozalishwa katika wilaya za  Mpwapwa, Kongwa, Kondoa,  Bahi na Chamwino mkoani Dodoma, ambapo kila kilo ya mtama ilinunuliwa kwa shilingi 550. "Mradi umekuwa na matokeo mazuri na umewezesha  kuboresha maisha ya wakulima wa mtama" aliongeza.

Kwa mujibu wa Msechu kampuni kwa sasa inanunua asilimia 74% ya malighafi zake nchini na imedhamiria kuongeza kiwango cha ununuzi wa malighafi nchini katika  miaka ijayo.TBL Plc imejipanga kuhakikisha inashirikiana na wakulima wa mtama wapatao 6,000 katika  msimu wa 2020-2021 ili kukidhi kupata mahitaji yake ya tani 10,000 za mtama kwa ajili za kuzalisha chapa zake za Eagle na Bingwa.

Akiongea katika mkutano huo wa tathmini,Mwakilishi wa WFP, Lusajo Bukuku alisema kabla ya kuanzishwa kwa mradi huo wakulima walikuwa wanazalisha magunia 3 hadi 4 ya mtama kwa ekari.Kutokana na kupatiwa mbinu bora za kilimo na usimamizi mzuri mavuno yao kwa sasa yameongezeka kufikia karibu magunia kati ya 10 hadi 11 kwa ekari.

Naye Mwakilishi wa Farm Africa ,William Mwakyami,alisema kupitia mradi huu,taasisi yao imesaidia kuwezesha wakulima wapatao 846 ambao wamenufaika kwa kujiongezea kipato kutokana na kuzalisha zaidi kulinganisha na kipindi cha nyuma kabla ya mradi na wameweza kuwa na soko la uhakika la mavuno yao.
 
Kaimu Afisa Kilimo wa Wilaya ya Kongwa, Bi Amina Msangi, amesema kabla ya kuanzishwa kwa mradi huu wakulima walikuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa soko la uhakika la mavuno yao. Alitoa wito kwa wakulima kuchangamkia  fursa hii ya soko la uhakika iliyopatikana ili iwasaidie kujikwamua kimaisha.

Mpango wa  TBL Plc wa kununua malighafi nchini ni moja ya mchango wa kampuni ambao unaenda sambamba kufanikisha jitihada za Serikali katika kukuza uchumi wa Tanzania.

Mwaka 2018, ABInBev ilijitoa kuwapatia ujuzi, kuwaunganisha na kuwawezesha kifedha wakulima mpaka kufikia mwaka 2025. Kutokana na mkakati huo,TBL Plc  imefanya uwekezaji wenye lengo la kuwainua wakulima wadogo nchini Tanzania kwa kuwaanzishia huduma mbalimbali-Kilimo Uza. 

Kutumiwa meseji za simu kuwapatia taarifa mbalimbali kama hali ya hewa, taarifa za masoko, ushauri wa kitaalamu. huduma ya mkopo wa pembejeo, mafunzo kuhusiana na masuala ya fedha na ununuzi wa pembejeo bora na matumizi yake, matokeo ya utafiti wa mbegu bora za mtama unaofaa kuzalishwa nchini, mbinu za kilimo cha kisasa sambamba na kuwasaidia katika kipindi chote cha msimu wa kilimo ili waweze kusimama na kufanya vizuri zaidi.
Share To:

Post A Comment: