Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

KATIBU Mkuu Wizara ya elimu, sayansi na teknolojia Dkt. Leonard
Akwilapo amewaasa baadhi ya wadhibiti ubora wa shule nchini
kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuacha lugha za vitisho kwa
wateja.

Dkt. Akwilapo amesema hayo katika ufunguzi wa mafunzo maalum kwa
wathibiti wakuu ubora wa Shule kanda na Wilaya zote Tanzania bara,
wapatao 217, yanayofanyika wilayani Bagamoyo kwa muda wa siku tatu .

Anasema, lengo la mafunzo ni kuwaongezea ujuzi wa masuala mbalimbali ya
utendaji katika utumishi wa umma na kuwasaidia wathibiti wakuu ubora
wa shule kuondoa ama kurekebisha changamoto za kiutendaji ambazo
zimekuwa zikiripotiwa kwa uongozi wa wizara mara kwa mara katika
maeneo wanayosimamia.

“Wizara imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wadau na watoaji wa
elimu kuhusu mwenendo usiofaa wa baadhi ya Wathibiti Ubora wa Shule
kutoa lugha za vitisho kwa wateja na wakati mwingine kuwaomba Rushwa
ili kufanikisha usajili wa Shule au Vyuo vyao .

"Hii ni kukiuka maadili ya utendaji katika utumishi wa umma kwa
kutozingatia sheria, kanuni na maadili ya utendaji katika utumishi wa
Umma na wadhibiti ubora wa elimu wanaofanya vitendo hivi waache mara
moja kwani taarifa zako zitakapotufikia hatutasita kukuchukulia hatua
za kinidhamu” Amesema Dkt. Akwilapo.

Mshiriki wa Mafunzo hayo Bi.  Tatu Tamizi Kutoka Wilaya ya Gairo
akizungumza kwa niaba ya Washiriki  wa mafunzo hayo amesema,
wanashukuru Wizara ya elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuwaandalia
mafunzo hayo ambayo wanaamini yatawaongezea weledi na ufanisi katika
utendaji kazi wao na hivyo kuboresha utoaji huduma za elimu nchini.
Share To:

Post A Comment: