Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akihutubia Wazee wa Makazi ya Sukamahela.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt ..Rehema Nchimbi pamoja na Kamishna kutoka Ustawi wa Jamii,  Naftari Ng'ondi wakikabidhi chakula kwa wazee hao.


Wazee wa makazi ya Sukamahela wakimsikiliza mkuu wa mkoa.


Wazee wa makazi ya Sukamahela wakimsikiliza mkuu wa mkoa.
Jengo jipya la utawala lililopo kwenye makazi ya Sukamahela.
 


Na Ismail Luhamba, Manyoni.


KATIKA kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee Duniani, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ametembelea makazi ya Wazee mkoani hapa yaliyopo Sukamahela Wilayani Manyoni na kuzungumza nao.

Akizungumza na Wazee hao juzi, Dkt. Nchimbi alisema Wazee ni tunu kwa Taifa kwani mawazo yao ndio yanayopelekea mafanikio makubwa hapa nchini.

Alisema kupitia serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli imejikita kuimarisha uchumi kwa lengo la kuwasaidia wananchi wakiwemo wazee ndio maana serikali ilianzisha makazi kwa ajili ya wazee ili iweze kuwatunza.

"Tarehe 01 oktoba kila mwaka ni siku ya wazee Duniani siku hii ikatukumbusha kuwatunza wazee wetu. familia zetu ziwatunze wazee wetu,kama unachangamoto ya kumtunza mzee wako nenda kwa viongozi wako,nenda kwa mkuu wa wilaya toa taarifa ili serikali iweze kukusaidia." alisema Dkt. Nchimbi. 

Aidha Dkt.Nchimbi  aliwakabidhi wazee hao zawadi mbalimbali ikiwemo mafuta ya kula,mchele,ndoo za maji, sukari, mbuzi kwa ajili ya kitoweo na sabuni huku akiwaambia kuwa serikali inatoa matibabu bure kwao,hivyo kama kuna baadhi ya madaktari kwenye Zahanati,Vituo vya afya na Hospitali za mkoa huo hawatekelezi jambo hilo watoe taarifa ili kutatua changamoto hiyo ikiwemo kuchukua hatua za kisheria.

"Serikali inawapenda sana ndio maana mpo na hapa tumeona imefanya ukarabati wa majengo yetu,tunahitaji mawazo kutoka kwenu ili na sisi tufike hapo mlipo." alisema Dkt. Nchimbi.

Awali akisoma taarifa ya Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Kamishina wa Ustawi wa Jamii Naftari Ng'ondi  alisema mpaka sasa serikali inatoa matunzo kwa wazee 281 katika makazi 13 ya wazee nchini ambapo eneo la Sukamahe ni moja ya makazi hayo.

"Hapa Sukamahe tunatunza jumla ya wazee 15, Wizara inajivunia kupata mafanikio katika maeneo mbalimbali ya utoaji huduma kwa wazee tunaowahudumia hapa nchini." alisema Ng'ondi.

Alisema serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya majengo ya makazi ya wazee kwa kufanya ukarabati wa majengo yaliopo na kuanzisha majengo mapya ambapo kwenye makazi ya Sukamahe serikali imejenga jengo la utawala kwa lengo la kuimarisha mazingira mazuri ya kazi kwa watumishi wa makazi hayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Makazi ya Sukamahela,  Andrea Yohana aliishukuru serikali kwa kuendelea kuwajali na kuwatunza wazee,na kuiomba serikali isichoke kuwatunza licha ya kuwa hawana uwezo wowote wa kuilipa.

"Tunaliombea taifa letu liweze kuvuka salama kwenye kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi kama alivyotuvusha kipindi cha Corona ili tuendelee kuishi kwa amani." alisema Yohana.

Share To:

Post A Comment: