Friday, 18 September 2020

TUNAHITAJI KURA NYINGI ZA RAIS MAGUFULI NA UDIWANI MIONO-RIDHIWANI KIKWETE


NA MWANDISHI WETU

MBUNGE Jimbo la Chalinze aliyepita bila kupingwa Mhe. Ridhiwani Kikwete ameomba Wananchi wa Miono kujitokeza kwa wingi kupiga kura za ushindi Oktoba 28, kwa kuwachagua Diwani na Rais watokanao na Chama Cha Mapinduzi CCM ilikuendelea kuleta Maendeleo.

Ridhiwani Kikwete amesema hayo  leo wakati wa mikutano yake ya ndani kwa Wajumbe wa CCM iliyofanyika katika vijiji vya Kweikonje, Masimbani na Kikaro-Miono Shule ambapo alisema Serikali inatambua maendeleo ndio maana Chama kimeweza kutunga sera zenye kuwafikia Wananchi wote bila kubagua.

"Miono inahitaji viongozi makini na viongozi hao wanatokana na CCM.

Tujitokeze kwa wingi Oktoba 28, kumchagua Diwani wetu  Juma Mpwimbwi na Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ilikuendelea kuleta maendeleo kwa Wana Miono." Alisema Ridhiwani Kikwete.

Alisema maendeleo hayo ni pamoja na kuboresha huduma za kijamii ikiwemo shule, Vituo vya afya sambamba na kuimalisha miundombinu ikiwemo barabara na mawasiliano.

"Natambua mahitaji makubwa huku Kweikonje ikiwemo suala la barabara ambayo ni kiungo muhimu kutoka Miono kwenda Masimbani hadi kuja huku Kweikonje ambapo kwa sasa tayari zabuni imetangazwa ili kuboreshwa." Alisema Ridhiwani Kikwete.

Akielezea suala la Vijana, ambapo amewataka vijana kuendelea kujiunga kwenye vikundi ilikupata mikopo ya mitaji isiyokuwa na riba ilikuendesha shughuli zitakazowapatia vipato.

"Halmashauri ya Chalinze imetenga Bilioni 3 na zaidi ya asilimia 80 fedha za mikopo zimeenda kwa makundi maalum ikiwemo Wamama ambao wamenufaika na mikopo hiyo isiyokuwa na riba.

Naombeni sana, Vijana baadala ya kuomba mipira na jezi basi muungane kwenye vikundi kupata mikopo hiyo itakayowasaidia kujiingizia vipato. Tunataka mfanye kazi muda wa kazi na jioni mujiingize kwenye michezo kuimalisha afya." alisema Ridhiwani Kikwete.

Kwa upande wake, Mgombea Udiwani wa Kata hiyo, Juma Mpwimbwi aliwaomba Wananchi wa Miono kuendeleza umoja ili CCM ipate ushindi wa kishindo.

"Tunaomba kura nyingi za ushindi Oktoba 28 ni kwa CCM. Tutaendelea kuunganisha Miono katika umoja wetu na kuleta maendeleo.  Nichagueni nafasi ya Udiwani na pia tujitokeze kwa wingi kumpigia kura Rais Dkt. Maguli." Alisema Juma Mpwimbwi.

Katika mikutano hiyo, Wananchi pia walipata nafasi ya kuuliza maswali pamoja na kutoa kero zao ambazo zilipokelewa kwa kufanyiwa kazi.

Mwisho.

No comments:

Post a comment