Mratibu wa Kitaifa wa Zao la Korosho kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele Mtwara, Dkt.Geradina Mzena (kulia), akiwaelekeza Afisa Kilimo na Mratibu wa Zao la Korosho Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Isabella Chilumba (kushoto) na  Afisa Kilimo wa Wilaya ya Gairo, Eunice Kyungai jinsi ugonjwa wa Ubwiriunga unavyoathiri zao la korosho. Mafunzo hayo kwa vitendo yalifanyika jana kwenye shamba la korosho la Shule ya Msingi Mnjilili wilayani Gairo, Morogoro.  

Mtafiti Mwandamizi na Mdhibiti wa Visumbufu vya Wadudu na Magonjwa kwenye zao la korosho, kutoka Tari- Naliendele  Mtwara, Dkt.Wilson Nene, akiwaeleza  Maafisa Ugani na Wakulima namna ya kudhibiti magonjwa mbalimbali ya zao hilo.
Mtafiti  kutoka Tari- Naliendele Programu ya Zao la Korosho, Kasiga Ngiha, akitoa mafunzo ya jinsi ya kuandaa shamba, kulipima na upandaji wa zao la korosho kwa Maafisa Ugani na Wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.
Maafisa Ugani na Wakulima wakijifunza kwa vitendo namna ya upimaji wa shamba la korosho kabla ya kupanda.
Afisa Kilimo kutoka Kata ya Madege Wilaya ya Gairo, Fideli Ntumo (Aliye chuchumaa akipima shamba kwa kamba katika mafunzo hayo ya vitendo. 
Mkulima Julius Senyagwa kutoka Kijiji cha Majawanga wilayani Kilosa,  akijifunza namna ya kuweka 'mambo' wakati wa mafunzo kwa vitendo ya upimaji wa shamba la korosho.
Afisa Kilimo kutoka Wilaya ya Gairo, Mary Gasper (kulia) na wenzake,  akijifunza namna ya kuweka 'mambo' wakati wa mafunzo kwa vitendo ya upimaji wa shamba la korosho. Kushoto ni Afisa Kilimo, Lucy Mushi na Jacquline Roland.
Afisa Kilimo kutoka Wilaya ya Gairo, Laya Abbas,  akijifunza namna ya kuweka mambo wakati wa mafunzo kwa vitendo ya upimaji wa shamba la korosho.
Mtafiti Mwandamizi na Mdhibiti wa visumbufu vya wadudu na magonjwa kwenye zao la korosho, kutoka Tari- Naliendele  Dkt.Wilson Nene, akiwaonesha kwa vitendo Maafisa Ugani na Wakulima namna ya kudhibiti magonjwa mbalimbali ya zao hilo.

Afisa Kilimo kutoka Wilaya ya Gairo, Nasibu Said, akishiriki mafunzo kwa vitendo kwa kuchimba mashimo kabla ya kupanda miche bora ya mikorosho katika shamba hilo lililopo shule ya Msingi Mnjilili, Gairo.


Mkulima  Elizabeth Senyagwa kutoka Gairo,  akishiriki mafunzo kwa vitendo kwa kuchimba mashimo katika shamba hilo la mfano la korosho la Shule ya Msingi Mnjilili.


Mtafiti  kutoka Tari- Naliendele Programu ya Zao la Korosho, Kasiga Ngiha, akitoa mafunzo ya jinsi ya kupanda mche wa korosho kwa Maafisa Ugani na Wakulima.


Mtafiti wa Kilimo kutoka  Tari Naliendele, Selemani Libaburu,  akitoa mafunzo ya jinsi ya kuchanganya viuatilifu na maji  kwa Maafisa Ugani na Wakulima kabla ya kupulizia kwenye mikorosho. 

Mtafiti wa Kilimo kutoka  Tari Naliendele, Selemani Libaburu, akionesha namna ya kupulizia viuatilifu kwenye mikorosho.


Afisa Kilimo kutoka Kata ya Magubike wilayani  Kilosa, Iston Kutita, akijifunza kwa vitendo namna ya kupulizia viuatilifu mikorosho.


Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Morogoro.

WAKULIMA wa zao la korosho mkoani hapa wameahidi kufanya mageuzi makubwa ya kilimo cha zao hilo baada ya kuhamasika na programu maalumu ya mafunzo ya nadharia na vitendo inayoendelea kutolewa na Wizara ya Kilimo kupitia Taasisi yake ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI)

Taasisi hiyo kupitia kituo chake cha Naliendele kwa sasa kinaendesha mafunzo ya kilimo bora cha zao la korosho kwa wakulima na maafisa ugani wa Halmashauri zilizo kwenye mikoa ya Kanda ya Kati, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kusini lengo likiwa kuongeza tija na kuinua kiwango cha uzalishaji wa zao hilo.

Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti wakati wa mafunzo hayo eneo la Shule ya Msingi Mnjilili, Mji Mdogo wa Gairo mkoani hapa wadau hao walisema mafunzo hayo yamekuja wakati mwafaka.

"Mafunzo haya yamenisaidia na kunipa mwanga wa namna ya kuboresha shamba langu la ekari mbili, kwa sasa nina matumaini makubwa ya kulima kitaalam zao hili." alisema mkulima wa korosho kutoka Dumila, Samwel Dede.

Mkulima mwingine Elizabeth Senyangwa kutoka Gairo alisema kabla ya kupata mafunzo hayo miongoni mwetu tulikuwa kwenye mtazamo wa kustawisha zao hilo kimazoea. Lakini kwa sasa nimejifunza mengi hasa kwenye eneo la udhibiti wa wadudu na magonjwa na namna bora ya kuandaa shamba langu.

Naye Afisa Ugani Elina Dastan kutoka Kilosa anaeleza kuwa anaona fahari kwa Taifa la Tanzania kupitia watafiti wake kuzidi kubuni teknolojia mpya kwa ustawi wa sekta ya kilimo nchini.

"Ugunduzi wa teknolojia za aina zote hizi za mbegu bora za korosho kutoka Tari ni fursa kubwa kwa wakulima na watanzania kwa ujumla." alisema Dastan.

Aidha, kutokana na hamasa iliyotawala wakati mafunzo yakiendelea, wadau hao wa zao la korosho walitaka kufahamu kwa kina ni aina ipi ya mbegu za korosho ambazo ni bora zaidi na zinazaa kwa wingi kama mkulima atahitaji kupata mavuno zaidi?.

Lingine lililojitokeza kwenye majadiliano ni je mbegu za zao hilo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo zinachukua muda gani hadi kuanza kuvunwa korosho yake sanjari na umakini wa palizi yake?

Na washiriki wa mafunzo hayo walitaka kufahamishwa endapo wanataka mbegu za Tari kwa haraka watazipataje na kwa utaratibu gani?.

Na zaidi wakionesha mwamko mkubwa walitaka kujua uhakika wa mwenendo wa soko kwa sasa...huku wale wengine waliopatiwa mbegu na Serikali huko nyuma wakitaka kuhakikishiwa ubora na uhalali wa mbegu hizo.

Akijibu maswali hayo Mratibu wa zao hilo kitaifa, Dkt Geradina Mzena alisema mbegu zote zilizogunduliwa na kufanyiwa utafiti na Serikali kupitia taasisi hiyo zina ubora na zinafaa kwa matumizi ya mkulima katika kupata tija inayostahili.

Huku Mtafiti kutoka Kituo cha Tari Naliendele Mtwara, Kasiga Ngiha akibainisha kuwa mbegu za korosho zinazozalishwa na kituo hicho huchukua kati ya miaka miwili mpaka mitatu kabla ya kukomaa na korosho yake kuanza kuvunwa.

Ngiha alisema mkulima anapaswa kuzingatia kanuni bora za kilimo cha zao hilo ili kuleta tija na ustawi, na anapofikia wakati wa kupalilia hupaswa kuwa makini kwa kuhakikisha jembe analotumia lisizame zaidi ya sentimeta 20 kinyume chake anaweza kujikuta akikata mizizi ya mkorosho inayoota kwa kwenda chini na ile inayotambaa.

Akifafanua utaratibu wa kupata mbegu hizo hususan kwa wakulima wa mkoa wa Morogoro, Dkt  Mzena alisema mkulima yeyote anayehitaji mbegu hizo awasiliane na Bwana Shamba aliye karibu naye, na yeye atawasiliana na Tari Naliendele ili kupatiwa huduma hiyo.

Aidha kwa wakazi wa mkoa wa Morogoro wanaweza kutumia kituo cha mauzo ya mbegu cha Tari kilichopo Bagamoyo maarufu 'Cash Development Centre (CDC)'

Akifafanua kuhusu uhakika wa soko la korosho Mzena aliwahakikishia wakulima kuwa zao hilo kwa miaka yote limeendelea kuwa ni 'dhahabu ya kijani' na soko lake halijawahi kuyumba.

Alisema zao hilo linauzwa kwa mfumo kamili unaosimamiwa hatua kwa hatua yaani mfumo wa stakabadhi ghalani sambamba na mkulima wa zao hilo kuendelea kuwa na fursa lukuki za kukopesheka kupitia taasisi za fedha.

Na kuhusu hoja iliyoibuliwa juu ya zile mbegu zilizotolewa na Serikali huko nyuma kipitia mabwana shamba alisema mbegu hizo zipo salama na zinafaa kwa matumizi.

Kwa upande wake Afisa Kilimo na Mratibu wa Zao la Korosho mkoani hapa Isabella Chilumba alisema azma ya mkoa huo ni kuzalisha tani 500 za korosho ifikapo 2023, huku msimu ujao 2020/21 wakitarajia kuzalisha tani 300 ya zao hilo.

Hata hivyo Chilumba alibainisha hatua kwa hatua maendeleo kadhaa ya ongezeko la uzalishaji wa zao la korosho kwa misimu 3 iliyopita, ambapo mwaka 2017/18 mkoa ulipata tani 63, na 2018/19 ulipata tani 155, mwaka 2019/20 kiwango hicho kiliongezeka na kufikia tani 181.5, huku shabaha ya taifa ni kufikia tani milioni 1  ifikapo 2023.

"Naamini kwa mafunzo haya yanayotolewa  na taasisi ya utafiti wa  kilimo, pamoja na stratejia zingine tulizonazo kama mkoa yatachochea kwa kiasi kikubwa kasi ya ongezeko la uzalishaji kwa tija na ubora." alisema Chilumba.

Share To:

Post A Comment: