Tuesday, 28 July 2020

WAGOMBEA NAFASI MBALIMBALI ZA UONGOZI WALIOSHINDWA KURA ZA MAONI WATAKIWA KUWA WATULIVU


 Katibu mwenezi na siasa wa CCM Mkoani Njombe Erasto Ngole ( aliyesimama) akiongea na wajumbe wa UWT wilaya hawapo pichani. Kulia kwake ni katibu wa CCM Ludewa Bakari Mfaume na katibu wa UWT Ludewa Flora Kapalia, na kulia kwake ni mwenyekiti wa UWT Ludewa Helena Msanga
 Wajumbe wa UWT wilayani Ludewa Mkoani Njombe wakisubiri kupiga kura za maoni kuwachagua madiwani viti maalum
 Katibu mwenezi na siasa wa CCM mkoa wa Njombe Erasto Ngole akiwa katikati ya wagombea wa kura za maoni viti maalum
 Katibu wa CCM wilayani Ludewa Mkoani Njombe Bakari Mfaume wakwanza kushoto akiwaonyesha kura zilizopigwa wagombea wa tarafa ya Liganga
 Wasimamizi wa kura za maoni viti maalum Ludewa, kutoka kushoto ni mjumbe Halmashauri kuu CCM mkoa wa Njombe Thobias Lingalangala, katibu wa CCM Ludewa Bakari Mfaume na Katibu wa jumuiya ya wazazi Ludewa Veronica Biria
 
Na Shukrani Kawogo

Wagombea wa nafasi mbali mbali za uongozi walioshindwa katika kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Njombe wametakiwa kuwa watulivu na kuendelea kukitumikia chama badala ya kuunda vikundi na kutaka kuhamia vyama vya upinzani.

Hayo ameyasema katibu mwenezi na siasa wa chama hicho mkoa wa Njombe Erasto Ngole alipokuwa akisimamia kura za maoni kwa madiwani wa viti maalum wilaya ya Ludewa mkoani humo.

Alisema kuwa amepata taarifa kuwa kuna baadhi ya maeneo kuna wagombea wa kura za maoni katika nafasi za udiwani ambao kura zao hazikutosha wameanza kuunda vikundi ili kuhamia upinzani kitu ambacho wanapoteza muda na kujichafua wao wenyewe.

“Nafasi ya uongozi ipo kwa ajili ya mtu mmoja sasa mmegombea watu zaidi ya ishirini anapopita mmoja nyie ambao hamjachaguliwa mnapaswa kuendelea kuunga mkono chama na si kuhama kwakuwa nafasi ya uongozi si ya kudumu hivyo itafika wakati aliyeko madarakani atatoka na kumuachia mwingine”. Alisema Ngole.

Aliongeza serikali ya awamu ya tano imejipanga vyema hivyo katika uchaguzi huu kwa mkoa wa Njombe hakuna kata hata moja itakayokwenda upinzani hivyo wanaotaka kuhamia upinzani wanajisumbua wenyewe na chama kitawashughulikia.

Aidha kwa upande wa katibu wa chama hicho wilayani Ludewa Bakari Mfaume amesema kuwa kwa wagombea ambao hawakuridhishwa na matokeo milango iko wazi kuleta malalamiko lakini wanapaswa kuwa na ushahidi wa kutosha juu ya malalamiko yao na chama kitayafanyia kazi malalamiko hayo.

Aliongeza kuwa kuna baadhi ya wanachama wameanza kuwashawishi wanachama wenzao wahamie upinzani ili kuungana na kupeperusha bandera za upinzani hasa katika tarafa ya Lignga pamoja na tarafa ya Masasi ambapo ametoa maagizo kwa madiwani waliopita katika kura za maoni wa maeneo hayo kushirkiana na viongozi na kuhakikisha fujo hizo haziendelei.

Katika uchaguzi huo wa kura za maoni za madiwani viti maalum walijitokeza wagombea 29 katika tarafa tano za wilaya hiyo ambapo kila tarafa ilitakiwa kutoa madiwani wawili kwa kupigiwa kura na wajumbe 319.

Wagombea waliofanikiwa kupita katika kura hizo katika tarafa ya Mawengi ni Mary Mapunda kura 120 na Angela Livato kura 108, Tarafa ya Masasi Grace Mapunda kura 186 na Leah Mbilinyi kura 148, tarafa ya Mwambao Reinada Tweve kura 161 na Yohana Gohele kura 150, tarafa ya Liganga Selina Haule kura 223 na Florencia Msemwa kura 167, tarafa ya Mlangali Averina Mgaya kura 290 na Agatha Kayombo kura 287.

No comments:

Post a comment