Mkuu wa MKoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akifunga  mafunzo maalum ya  siku sita kwa wadau zaidi ya 300 kutoka katika mikoa mbalimbali nchini  yaliyokuwa yameandaliwa na Baraza la Taifa  la watu wanaoishi na  virusi vya UKIMWI (NACOPHA) kupitia “Mradi wa Hebu Tuyajenge” unaotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano 2019-2024, unaofadhiliwa na  Shirika la Marekani  la  Maendeleo ya Kimataifa (USAID) katika mikoa 22 Tanzania Bara. kushoto Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Rahabu Mwagisa, Kulia Mkurugenzi wa Utatifi wa NACOPHA  Pantaleo Shoki




>Awataka wenye virusi kufanya kazi bila hofu

>Awaonya wanaomchokoza,asisitiza hatatia nia
Na John Mapepele 
 
 Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi amempongeza Rais Magufuli kwa kuvunja rekodi ya  maendeleo kabla ya mwaka 2025 na kuifanya Tanzania kuingia kwenye nchi za uchumi wa kati duniani Julai Mosi mwaka huu.  
Huku akiwahimiza watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI nchini  kufanya kazi kwa  bidii bila kuwa na hofu sambamba na kumtanguliza Mungu na kutumia fursa za mikopo inayotolewa na Serikali ya Awamu ya Tano ili  ku kuinua hali za maisha na kuongeza pato la taifa kwa ujumla
Dkt. Nchimbi ameyasema hayo leo katika Mji Mdogo wa Manyoni mkoani  Singida alipokuwa akifunga  mafunzo maalum ya  siku sita kwa wadau zaidi ya mia 3 kutoka katika mikoa mbalimbali nchini  yaliyokuwa yameandaliwa na Baraza la Taifa  la watu wanaoishi na  virusi vya UKIMWI (NACOPHA) kupitia “Mradi wa Hebu Tuyajenge”.
Mradi huo unaotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano 2019-2024,unaofadhiliwa  na  Shirika la Marekani  la  Maendeleo ya Kimataifa (USAID) katika mikoa 22 Tanzania Bara.
Amesema kwa sasa Serikali ya Awamu ya Tano imepiga hatua kubwa ya kupiga vita unyanyapaa dhidi ya watu wanaishi na virusi vya UKIMWI na kwamba watu wote wana haki na fursa sawa  mbele ya Serikali yao hivyo hakuna sababu ya  wao kuendelea kujinyanyapaa  wenyewe  na badala yake wawe walimu wa kuwaelimisha wengine kwenda kupima na kutambua hali zao  na kuendelea kuchapa kazi ili kuinua uchumi wan chi yetu.
“Kubwa ndugu zangu hapa ni  kumtanguliza  Mungu mbele, kutoa hofu na  kuachana  na mambo yote ambayo yanapelekea  kudhoofu kwa afya zetu kama vile unywaji wa pombe  hata kama wake zetu wanapika  kwa ajili ya biashara na badala yake tutumie juisi lishe za matunda ya asili kama vile  Sasati, Ubuyu na Ukwaju” amesisitiza Dkt. Nchimbi
Umewaelekeza  Wataalam wa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Singida kuangalia namna  ya kuja na mikakati madhubuti ya kiuendelevu ya kuwakopesha wanaoishi na UKIMWI  ili kuwaletea maendeleo huku akisisitiza kuwa  Mkoa wake utaendelea kutekeleza mikakati iliyojiwekea ya kuinua maisha  ya wanainchi wake ikiwa ni pamoja na mkakati wa kuwavusha salama mama na mtoto.
Aidha ameweka msimamo wake wa kutokuonesha nia yeyote ya kuomba ridhaa ya kugombea Ubunge katika uchaguzi wa mwaka huu huku akiwaonya watu ambao wamekuwa wakianza kudanganya kuwa atagombea ambapo alisisitiza kuwa nafasi hiyo ya ukuu wa Mkoa aliyopewa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli ni ya heshima kubwa.
“Naomba niliseme  hili, na tayari nimeshalisema mara kadhaa  hata hivi karibuni nilipokuwa nyumbani kwangu, kijijini Matufa,  Babati Manyara nilipo hudhuria mazishi ya mtoto wa Kaka yangu aliyefariki kwa ajali ya Pikipiki kwamba nilikwenda kuungana na familia yangu katika msiba wa kijana wetu na si vinginevyo. Ninaridhika sana na nafasi hii niliyo nayo ya ukuu wa Mkoa" alisema Dkt. Nchimbi huku akishangiliwa na umati wa  wadau wa mafunzo hayo
Baadhi ya waombolezaji wamesikika kupongeza msimamo wa kiongozi huyo, huku wakisema  kuwa Msimamo huo unapaswa kuigwa na viongozi wengine  kwa kuwa umejikita katika kuwaletea maendeleo wananchi badala ya kuwa na tamaa za madaraka.
“Binafsi nampongeza sana Mama Nchimbi  kwani kwa muda wote amekuwa aking’ang’ana na kuwaunganisha watu wote bila kujali dini wala rangi kwa, hata sisi leo ametutia moyo sana kiasi kwamba  baada ya kutoka hapa tumekuwa na nguvu mpya  ya kuchapa kazi na kushirikiana na Serikali yetu ya  kujiletea maendeleo Zaidi ili tutoke katika nchi za uchumi wa kati na kwenda katika nchi tajiri duniani na tuna imani kubwa chini ya Rais wetu Magufuli tutafika” amesema Amina  Huredi ambaye ni Mshiriki wa mafunzo hayo kutoka Singida
Mkurugenzi wa Utatifi wa NACOPHA  Pantaleo Shoki  amemshukuru Mkuu wa Mkoa na kumhakikishia kuwa  wataendelea kushikiana na Serikali ili kuhakikisha kuwa malengo ya Mradi huo yanatimia kama yalivyopangwa.
Shoki  amesema Mradi  unalenga kufikia Mkakati wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI(UNAIDS) wa 95-95-95 yaani  asilimia 95 ya watu wote wanaoishi na maambukizi ya VVU wawe wamepima na kugundua afya zao,asilimia 95 ya watu wote waliopimwa na kukutwa na maambukizi wawe wameanza tiba na asilimia 95 walio kwenye tiba wawe wamefubaza virusi hivyo ifikapo 2030
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: