Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amezindua Chuo cha Ufundi Stadi Nyamidaho kilichopo Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma.

Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi, Profesa Ndalichako amesema uanzishwaji wa Chuo hicho ni mwendelezo wa utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga vyuo vya  ufundi stadi katika kila Wilaya Nchini ili kupeleka huduma hiyo karibu na Wananchi na kuwapatia ujuzi vijana wa kitanzania.

Ndalichako amesema Chuo cha Nyamidaho kimetokana na majengo yaliyokuwa yakitumiwa na Taasisi ya World Vision ambapo Serikali imekarabati majengo yaliyokuwepo na kujenga mengine mapya.

Waziri Ndalichako ameeleza kuwa jumla ya Shilingi milioni 534 zilitolewa  kwa ajili ya  kazi hiyo na kwamba zimetumika milioni  477 hadi ukamilishaji. Aidha ameridhia ombi la kiasi kilichobaki kutumika kuanzisha ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kiume.

Ameongeza kuwa katika Mwaka 2019/20  vyuo 10 vya Halmashauri za  Wilaya vimejengwa na kuanza kutoa mafunzo.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Emmanuel Maganga ameishukuru Wizara ya Elimu kwa kukamilisha ujenzi wa chuo hicho na amewataka wakazi wa kijiji cha Nyamidaho kuhakikisha vijana wao hasa wa kike wanajiunga na chuo hicho.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya VETA, Peter Maduki ameishukuru Serikali  kwa kuendelea kuimarisha Elimu ya Ufundi nchini  na kuongeza kuwa Chuo hicho kipya kina wanafunzi takriban 70. Aidha ameagiza Uongozi wa VETA kutoa bure mafunzo ya kozi ya uwashi kwa wanafunzi wanaotoka Nyamidaho.
Share To:

Post A Comment: