Monday, 15 June 2020

WATUMISHI WAWILI WA TRA MANYARA WAPANDISHWA KIZIMBANI KWA MAKOSA YA RUSHWA.


Na John Walter-Babati
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara imewafikisha katika Mahakama ya wilaya ya Babati, Eva Joseph Mtandika na Jackline Leonard Manjira kujibu mashtaka ya kuomba na kupokea hongo ya  shilingi Milioni moja (TSh.1,000,000/=)   kutoka kwa mfanyabiashara mjini Babati.
Watuhumiwa hao  wamefikishwa mahakamani hapo  kwa mara ya kwanza leo Juni 15 katika mahakama ya wilaya hiyo  kwa makosa mawili ya kuomba na kupokea Rushwa kutoka kwa mfanyabiashara mjini Babati.
Katika shtaka hilo la jinai Namba 108 ya mwaka 2020, Upande wa mashtaka ukiongozwa na mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Martin Makani,  ulidai  mbele ya mahakama kuwa washtakiwa hao kwa kushirikiana walipokea hongo hiyo toka kwa mfanyabiashara huyo kati ya Juni 6 na Juni 11,2020 mjini Babati  ili wasimpige faini kwa kutotumia mashine ya EFDs na kumtuhumu kuwa hatoi risiti kwa wateja.
Mwendesha mashtaka Makani alisema washtakiwa hao walitenda makosa hayo  kinyume  na kifungu cha 15 (1) (a) na kifungu cha 15 (2) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007 namba 11.
Hata hivyo washtakiwa wote wamekana mashtaka hayo yanayowakabili ya kuomba na kupokea hongo ya shilingi Milioni Moja.
Hakimu Victor Kimario aliwataka Washtakiwa  hao kila mmoja awe na mdhamini  mmoja ambaye atasaini hati ya dhamana ya shilingi Milioni mbili kila mdhamini ambao wote walikidhi vigezo hivyo na w kwa dhamana.
Kesi inayowakabili watumishi  hao imeahirishwa  hadi Julai 16 mwaka huu itakapotajwa tena kwa ajili ya kusikilizwa.No comments:

Post a Comment