Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mara

Uongozi wa Mkoa wa Mara umesisitiza kuendelea kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kuhusu wanunuzi binafsi wakati akizungumza na wananchi wa Kyaka, Rwamisheye, Kemondo Muleba, Nyakabango na Kyamyorwa mkoani Kagera tarehe 11 Julai 2019.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe Adam Malima leo tarehe 2 Juni 2020 wakati akizungumza Kwenye kikao kazi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Prof Jamali Adam ofisini kwake Mjini Musoma ambapo amesisitiza kuwa wanunuzi binafsi wataruhusiwa kununua Kahawa kupitia Vyama vya Ushirika badala ya kwenda moja kwa moja kwa wakulima.

Amesema kuwa serikali iliamua kuanzisha Ushirika kwa ajili ya wakulima ili waweze kuuza mazao yao kwa bei nzuri hivyo wanunuzi binafsi ni ruksa lakini wanapaswa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

"Uuzaji wa Mazao ya wakulima kupitia Vyama vya Ushirika tumeuweka ili kama wakulima wakiibiwa au kupunjwa sisi iwe rahisi kumpata muhusika na tunachukua hatua kali dhidi ya wote watakaofanya ubadhilifu, lakini tukimkuta mnunuzi binafsi ameingia mpaka shambani ni kama ameingia chumbani atapata balaa" Amesisitiza Mhe Malima

Mkuu huyo wa Mkoa wa Mara Mhe Adam Malima ameitaka Bodi ya Kahawa kutafuta wanunuzi binafsi kadri iwezavyo ili kuongeza ushindani na wakulima waweze kupata bei nzuri kwani jambo hilo itasaidia kukabiliana na unyonyaji dhidi ya wakulima wa kahawa pamoja na Mazao mengine Mkoani Mara.

"Mkulima yoyote akisikia bei nzuri ya kahawa lazima atauza hawezi kwenda Kwenye bei ndogo wakati ameona kuna mahala kuna bei nzuri inayoendana na jasho lake" Amesema Mhe Malima

Pamoja na mambo mengine Mhe Malima ameipongeza Bodi ya Kahawa kwa kutoa Miche 40,000 kwa ajili ya mkoa wa Mara huku akiisisitiza umuhimu wa Bodi hiyo kuwaongezea wakulima miche mingi zaidi ili kuongeza Uzalishaji wa kahawa nchini.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania Prof Jamal Adam amesema kuwa Bodi ya Kahawa imejiwekea malengo muhimu ya kuongeza Uzalishaji wa kahawa nchini, kuhakikisha kunakuwa na Bei nzuri, na kujenga mazingira bora ya Biashara kwenye tasnia ya kahawa.

Pia ameongeza kuwa Bodi ya Kahawa itaendelea kusimamia na kutekeleza maagizo ya serikali ikiwemo upatikanaji wa Miche Bora kwa wakulima, Malighafi Kwenye viwanda vya kahawa na kuhakikisha mkulima anapata bei nzuri kupitia kuongeza ushindani Kwenye soko la kahawa la awali na soko la pili.

Kadhalika, amewawasisitiza wakurugenzi wa Halmashauri mbalimbali nchini walioombwa vibali na wanunuzi binafsi na wenye viwanda kufanya hivyo kwa wakati ili Bodi iweze kutoa leseni mapema   

Share To:

Post A Comment: