Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe amewataka Watanzania kuwekeza katika sekta ya viwanda vinavyotumia malighafi za ndani.
Prof. Shemdoe aliyasema hayo Mkoani Simiyu alipokuwa katika ziara ya siku moja kutembelea Viwanda katika Mkoa huo. Katika ziara hiyo Katibu Mkuu na ujumbe wake walipata fursa ya kutembelea kiwanda kipya cha kuzalisha mafuta ya alizeti cha cha Bugari Investment Ltd kinachomilikiwa na Mtanzania kwa asilimia 100.
Prof Shemdoe alisema Bw. Bugari ameonyesha umuhimu wa kuwa na malengo katika kutekeleza jambo lolote.
 “ukiwa na malengo unaweza kufanya kitu chochote, hivyo natoa rai kwa watanzania wengine ambao wanaweza kuiga mfano huu  kufika mahali hapa na kujifunza, maana yote yanawezekana ukiweka nia”.
Kiwanda cha Bugari Investment Ltd  kimejengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 2  kinatarajiwa kutoa ajira kwa Watanzania 65 ikiwa ni  ajira za kudumu na za muda pamoja na kuchangia mapato kwa Serikali kupitia kodi mbalimbali.
Prof Shemdoe aliishukuru Serikali ya Mkoa kwa kumpa ushirikiano mwekezaji huyo na kumuwezesha kufanikisha kutimiza azma yake ya kujenga kiwanda. Pia alizishukuru Taasisi za fedha kwa kumuamini na kumpatia mkopo uliofanikisha kujenga kiwanda hicho.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Bw. Festo Kiswaga alisema wananchi wa Simiyu na mikoa ya jirani wamepata uhakika wa soko la alizeti kwa kuwepo kiwanda hicho.
“Tumekuwa tukiwasisitiza wananchi kulima, lakini changamoto iilikuwa upatikanaji wa masoko, hivyo uwepo wa kiwanda hiki utakuwa ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Mkoa huu na mikoa jirani’’.
Aidha alitoa wito kwa wananchi wa bariadi kuendelea kuzalisha alizeti kwa wingi ili kiwanda kiendelee kupata malighafi ya kutosha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bw. Nkuba Bugari alisema ujenzi wa kiwanda hicho umeanza mwaka 2015 na upo katika hatua za mwisho na ujenzi na kinatarajiwa kukamilika na kuanza uzalishaji mapema hivi karibuni.
Bugari alisema wazo la kujenga kiwanda hicho alipata  baada ya kupata hamasa kutoka kwa Mhe. Rais   Dkt. John Joseph Magufuli alipotoa rai kwa Watanzania kujenga viwanda.
“Ndugu Watanzania wezangu tusiache bahati hii ya kuwa na Mhe. Magufuli, ni kwa namna gani Mhe. Rais anajitoa kwa ajili watanzania katika kufanikisha Tanzania ya Viwanda”.
Anasema mashine zilizofungwa katika kiwanda hicho zina uwezo wa kuchakata mbegu za alizeti, pamba na karanga.
 Aliongeza kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata tani elfu arobaini na nane  za mbegu za alizeti. Hivyo lengo lao ni kushika soko la ndani pamoja kuuza mafuta hayo nje ya nchi ya Tanzania.Aidha aliwasisitiza watanzania kuwa na uthubutu katika kutimiza malengo mbalimbali.
Share To:

Post A Comment: