Na. Majid Abdulkarim

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani Jafo ameitaka Tume ya Utumishi wa Walimu kutatua changamoto na malalamiko ya walimu ikiwemo kubadilishwiwa mishahara baada ya kujiendeleza kielemu pamoja na manung’uniko mengine ili kuwatia moyo walimu katika kutimiza majukumu yao.

Kauli hiyo ameitoa jijini Dodoma wakati wa kuteuliwa na kuapishwa kwa wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Walimu .

Mhe. Jafo amesema kuwa Tume hiyo ndani ya wiki moja ikafanyie kazi malalamiko ya muda mrefu ikiwemo walimu kuchelewa kupandishwa madaraja baada ya kujiendeleza pamoja na kushughulikia mashauri ya rufaa ili walimu waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Amesisitiza kuwa Tume hiyo inatakiwa kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu hasa katika kushughulikia Ajira na Usajili, kupandisha madaraja, kubadilisha cheo walimu waliojiendeleza kimasomo pamoja na kusimamia maadili na nidhamu ya Walimu.

“Pamoja na mazingira magumu na changamoto naomba nikiri kwamba Tume ya Utumishi wa Walimu imefanya kazi kubwa tangu ianzishwa mwaka 2016 hadi sasa nendeni kaendeleze kasi ile ile mkawe sikio la walimu na kusimamia nidhamu ya walimu ili kuleta utendaji bora katika kutekeleza majukumu yao”, amesema Mhe. Jafo.

Aidha Mhe. Jafo ameitaka Tume hiyo kufanya kazi katika kanuni, miongozo na Taratibu zilizopo ili kuleta uwajibikaji katika shughuli za walimu hapa nchini.

Aidha mhe. Jafo ametoa wito kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo Prof. Willy Lazaro Komba kutoa ushirikiano kwa wajumbe wake ili kuweza kufanyikisha shughuli za utendaji katika ubora unaohitajika na walimu wanao wahudumia.

Wakati huo huo Mhe. Jafo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa maono yake juu ya kupambana na janga la Corona kwa kutozuia shughuli za watanzania ila kuwataka kuchukua taadhali na wananchi kuendelea na uzalishaji wao katika kutafuata kipato chao.

“Natoa rai kwa watanzania kuendelea kujifukizia (kupiga nyungu) kwa awamu ya pili ili kuimarisha afya zao zaidi na kupambana na kupambana na corana kwani vita hii haichagui siraha” alisisitiza Jafo.

Naye Mwenyekiti wa Tume hiyo Prof. Willy Lazaro Komba akitoa neno la shukurani amesema kuwa watatekeleza majukumu yao ipasavyo ili wanao wahudumia kupata huduma bora wanazotarajia kutoka kwao.

“Tuko tayari kuanza kazi ili kuwatumikia tunao waongoza na kufanikisha ubora katika shughuli za Walimu kote Nchini” ameeleza Prof. Komba.

Prof. Komba ametoa wito kwa wajumbe kutoa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Awali akitoa neno la ukaribisho Katibu Ofisi ya Rais,Tume ya Utumishi wa Walimu Bi. Winfrida Rutaindurwa alieleza kuwa tangu Tume ianze kutekeleza majukumu yake mwaka 2016 walimu 11,581 wameajiriwa, 14,507 walisajiliwa, 20,501 walithibitishwa kazini, 123,000 walipandishwa vyeo, 5,760 walibadilishwa vyeto baada ya kujiendeleza na walimu 20,316 wamestaafu na kuandikiwa vibali vya  kustaafu kazi.

Jufuatia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Josedph Magufuli kumteua Dkt. Willy Lazaro Mbuju Komba kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Selemani Jafo ameteua na kuwaapisha wajumbe nane wa TSC.

MWISHO
Share To:

Post A Comment: