NA HERI SHAABAN
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais  Muungano na Mazingira Musa Zungu amekabidhi simtanki kwa wafanyabiashara wa Masoko  yaliopo Jimbo la Ilala kwa ajili ya  kunawa mikono  ili wananchi waweze kujikinga na ugonjwa wa corona.


Simtanki hizo  zimetolewa na Jumuiya ya Wafanyabishara Wazalendo Tanzania  katika juhudi za kuunga mkono serikali na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.


Akikabidhi msaada huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mussa Zungu aliwataka Watanzania kufuata maelekezo ya serikali katika kuchukua hatua ya kujilinda kuhusiana na ugonjwa wa corona.

"Nawaomba Watanzania tutenge muda kwa ajili ya kusikiliza taarifa za habari zinazotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika kujilinda na ugonjwa huu hatari  wa corona " alisema Zungu.

Zungu aliwataka wananchi kila wanapofika maeneo ya masoko kunawa kila wakati na kuepuka kukaa sehemu za mikusanyiko ya watu wengi.

Zungu aliwataka Wajumbe wa Kila kata kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na ugonjwa huo.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wazalendo Tanzania Abdulsamad Abdulrahim alisema wanaunga mkono juhudi za Rais katika kupiga vita ugonjwa wa corona.

Mwenyekiti Abdulsamad alisema wametenga mapima 1000 kwa ajili ya kuisaidia serikali ambapo kila mkoa watafika.


Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Ilala Said Sidde amewataka wananchi kupunguza safari zisizo za lazima ,Wafanyakazi  kufanya kazi za uzalishaji katika kukuza uchumi wa nchi ili kuunga mkono juhudi za Rais kujenga Tanzania ya viwanda.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM kata ya Kivukoni Sharik Choughule amempongeza Waziri Zungu katika kujali afya za wananchi wanaofuata huduma soko la samaki Feri halmashauri ya ILALA.


Matanki hayo yalikabidhiwa  katika soko la Kimataifa la Feri,  Muhimbili kwa Afisa Mtendaji,Kariakoo Jumuiya ya Wafanyabiashara  Wamachinga, Soko la Mchikichini na soko la Ilala Boma ambapo walipokea viongozi wa maeneo hayo.


Mwisho
April 11/2020
Share To:

msumbanews

Post A Comment: