MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa aliyekuwa Mhariri wa gazeti la Mawio, Jabir Idrissa anayekabiliwa na kesi ya uchochezi pamoja na wenzake watatu aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lisu yupo kwenye uangalizi huko Visiwani Zanzibar, (karantini).

Wakili wa serikali, Sylvia Mitanto amedai hayo leo Aprili 23,2020 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kusikilizwa lakini mshitakiwa Idrissa yupo karantini na Lissu hayupo mahakama.

Mbali na Idrissa, na Lisu washitakiwa wengine ni aliyekuwa Mhariri wa gazeti la Mawio, Saimon Mkina na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

"Mheshimiwa,  kesi imekuja kwa ajili ya kusikilizwa lakini mshitakiwa Idrissa yupo karantini na Lissu hayupo mahakamani na hakuna taarifa zozote mpya juu ya kupatikana kwake.

Hata hivyo wadhamini wa Lissu,  Robert Katula na mwenzake walikuwepo mahakamani hapo.

Kufuatia taarifa hiyo, Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 21 kwa ajili ya kutajwa na Juni 17, mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.

Katika kesi hiyo washtakiwa wote wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwemo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 jijini  Dar es Salaam, washitakiwa, Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Pia, Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Aidha mshitakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokua na taarifa za uchochezi.

Inadaiwa mshitakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Mbali na mashitaka hayo washitakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016, Dar es Salaam, bila ya kuwa na mamlaka yoyote, waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: