Tuesday, 21 April 2020

Halmashauri ya Meru Yatumia Mil. 308 kutekeleza miradi ya Maendeleo.

 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ndg. Emmanuel Mkongo amesema Halmashauri hiyo katika kuunga mkono jitihada za wananchi kutekeleza miradi  ya maendeleo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 ilitenga kutoka katika makusanyo ya mapato ya ndani jumla ya shilingi milioni 515 na kutumia shilingi milioni 308 katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ununuzi wa vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba 21 vya madarasa na vyumba 3 vya maabara sambamba na ununuzi wa viti na meza ikiwa ni mkakati wa Halmashauri hiyo kuendelea kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu kwa kukamilisha vyumba vya madarasa na maabara ili kutatua changamoto ya msongamano wa wanafunzi kutokana na ufaulu mkubwa wa wanafunzi walioingia kidato cha kwanza mwaka huu na mkakati wa kuboresha ufundishaji wa masomo ya Sayansi.

Aidha , Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya milioni 18,961,020.06 kwa Shule ya Sekondari Maroroni na Sing'isi kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na maabara, Mkongo amesema vifaa hivyo vimegawanywa kwenye Kata zote 26 kwa kutoa kipaumbele kwa Kata ambazo Wananchi wake wameonesha juhudi za kuchangia ujenzi wa miradi ya maendeleo  akitolea mfano Kata ya Maroroni na Sing'isi na kutoa wito kwa wananchi wa Kata nyingine kufanya vizuri zaidi.

Aidha, Mkongo ameongeza  fedha hizo  jumla ya Shilingi milioni 308 za Mapato ya Ndani ya Halmashauri na  Shilingi Milioni 50,666,300 za mfuko wa kuchochea maendeleo ya jimbo ambao Mwenyekiti wa Kamati ya ya Mfuko huo ni Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki  Dkt. Danielson Pallangyo zimechochea kwa kiasi kikubwa ujenzi na ukamilishaji wa Miundombinu hiyo.

 Aidha, Mtendaji wa Kata ya Maroroni Bi. Lyidia Sarakikya amemshukuru Mbunge Dkt.Pallangyo na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru kwa kutoa mbao, bati na mifuko ya saruji kwaajili ya kukamilisha vyumba 3 vya madarasa kwani imewatia wananchi moyo kwa kupunguza  ukali wa michango.

Naye Mkuu wa Shule ya sekondari Maroroni ameishukuru Serikali na kutumia fursa hiyo kutoa wito kwa wazazi kutokubweteka kipindi ambacho shule zimefungwa badala yake wawasimamie wanafunzi kufanya mazoezi yaliyotolewa kwani shule hiyo iliwaandalia majaribio na masomo kwa kifurushi kilichopewa jina la HOME PACKAGE.

No comments:

Post a comment