Thursday, 26 March 2020

Waziri Ndalichako Aahidi kuunga Mkono Juhudi za Wabunge

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknojia Profesa Joyce Ndalichako akisikiliza maelezo juu ya maendeleo ya ujenzi wa shule maalum ya sekondari ya wasichana inayojengwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Wilayani Chamwino jijini Dodoma.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndungai akitoa ufafanuzi juu ya maendeleo ya ujenzi wa shule maalum ya wasichana inayojengwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jijini Dodoma.
Muonekano wa baadhi ya majengo ya shule ya sekondari maalum ya wasichana inayojengwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Chamwino Jijini Dodoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ameahidi kuunga mkono juhudi za wabunge katika ujenzi wa shule maalum ya Sekondari ya wasichana inayojengwa katika Kata ya Kikombo wilayani Chamwino, Mkoani Dodoma na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Profesa Ndalichako ametoa ahadi hiyo alipotembelea shule hiyo akiongozana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai ili kujionea maendeleo ya ujenzi huo ambapo amesema Wizara itatoa mchango katika kuunga mkono ujenzi wa shule hiyo ambayo ujenzi wake ni alama kubwa itakayoachwa na Bunge la kumi na moja chini ya uongozi wa spika Ndugai.

"Nimefarijika sana na kazi hii yenye ubora wa hali ya juu na nitaongea na wenzangu Wizarani ili tuone namna nzuri ya kutoa mchango wetu ili kuunga mkono kazi hii kubwa inayofanywa na Bunge. Mchango wetu utaangalia namna ya kuongeza majengo kwani eneo ni kubwa, natumai tukiongeza majengo hayo itaongeza idadi ya wanafunzi watakaokuwa wanadahiliwa katika shule hii,” amesema Profesa Ndalichako.

Profesa Ndalichako amesema amefurahishwa kwa jinsi Bunge hilo lilivyoamua kujenga shule kwa ajili ya wanafunzi wa kike kwani ni fursa kubwa kwa wanafunzi hao kupata elimu. Katika ziara hiyo Ndalichako ambae aliongozana na Kamisha wa Elimu, Dkt. Lyabwene Mtahabwa na Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora wa Shule, Euphrasia Buchuma amewaagiza kuanza hatua za ukaguzi wa shule hiyo kutoa ushauri ili usajili ufanyike kwa wakati pindi itakapokuwa imekamilika.

Naye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano waTanzania, Mhe. Job Ndugai amesema wabunge wa Bunge la 11 wamejitolea kuchangia ujenzi wa shule hiyo pamoja na kufanya shughuli mbalimbali za kuhamasisha uchangiaji ili kutimiza lengo hilo.

Mhe. Ndugai amesema shule hiyo inayojengwa itakuwa na miundombinu yote na imezingatia viwango na mwongozo wa serikali. Shule hiyo inatarajiwa kuchukua wanafunzi 320 wa Kidato cha tano na sita na ina miundombinu yote ikiwemo madarasa, maabara, mabweni, bwalo la kisasa la chakula, vyoo vya mfano, ofisi za walimu, jengo la utawala, maktaba yenye miundombinu ya TEHAMA na chumba cha afya.

No comments:

Post a Comment