Wazazi Mkoani Mbeya wamepewa tahadhali ya kuwa makini na watoto wao wadogo ikiwa ni pamoja na kuwawekea uangalizi mzuri kwa muda wote ili kuepuka madhara yanayoweza kuwapata watoto hao wanapokuwa wenyewe hasa katika kipindi hiki cha mvua nyingi.

Kutokana na mvua kubwa zinazonyesha mfululizo mkoani hapa maeneo mengi hasa jijini Mbeya kumekuwa na madimbwi ya maji sambamba na mifereji inayotiririsha maji kwa kasi kutokana pia na chemichemi baada ya sehemu kubwa ya ardhi kuwa oevu hatua inayohatarisha zaidi usalama wa watoto.

Kamanda wa polisi mkoani Mbeya,Ulrich Matei amesema kutokana na hali iliyopo ya mvua kubwa kunyesha kila mzazi na mlezi anapaswa kuongeza umakini zaidi katika uangalizi wa watoto wadogo hasa waliofikia hatua ya kutambaa na kutembea kwakuwa maji ya mvua yanaonekana kuhatarisha maisha yao.

Ulinzi pia umesisitizwa na jeshi hilo kwa wanafunzi wadogo hasa wa madarasa ya awali wanapokwenda na wanapotoka shuleni kuwa na waangalizi wa uhakika kwakuwa wapo baadhi wanaopita katika njia zinazokatisha vijito au mitaro ya maji sambamba na jirani na madimbwi na visima ambavyo wakati wa mvua kubwa kutokana na umri wao mdogo si rahisi kutambua hatari inayokuwepo sehemu husika.

Kamanda Matei alisema jana kuwa kwa kipindi cha hivi karibuni, kumekuwa na matukio ya watoto wadogo kufariki kutokana na kutumbukia katika visima vya maji, mabwawa, madimbwi yenye maji au katika mito pindi wanapovuka kuelekea Shuleni au wanapocheza.

“Katika msimu huu wa mvua kubwa na nyingi zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali mkoani kwetu na maeneo jirani tayari zimeanza kuleta madhara kwa binadamu hasa watoto wadogo.Yapo mambo ya kuepuka hasa matumizi ya vifaa vya umeme kama vile redio, tv na simu za mkononi wakati mvua kubwa zinazoambatana na radi zikinyesha.”

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa tahadhari kufuatia matukio ya kufa maji yanayosababishwa na uzembe wa kutovaa maboya wakati wanapoingia majini, mtoni au ziwani. Aidha kufuatia mvua zinazonyesha nawasihi wazazi kuwapeleka watoto wadogo shuleni na kuwapokea ili kuwalinda dhidi ya madhara ya kutumbukia katika maji.”alisisitiza Matei.

Kamanda huyo pia alitoa angalizo kwa watu wanaofanya shughuli za uchimbaji madini katika migodi, kuchukua tahadhari za kiusalama ili kuepuka ajali katika maeneo hayo hasa za kuangukiwa vifusi vya udongo huku pia akiwataka kufukia mashimo yasiyokuwa na dhahabu kwani ni hatari kwa watoto na watu wazima pindi yanapojaa maji.

Aidha kamanda Matei aliisihi jamii nzima kutambua umuhimu wa kila mmoja kuwajibika katika malezi ya watoto wote kwa kuzingatia kuwa mtoto ni wa jamii hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kuwajibika katika ulinzi na usalama wao kwa katika maeneo yenye mito au maji mengi ili kuepuka madhara yanayoweza kuwapata.

Wakati jeshi la polisi likitoa thadhari hiyo,baadhi ya wadau mkoani hapa nao walisema ipo haja kwa wakazi wanaomiliki visima vya wazi kuhakikisha wanavijengea uzio kwakuwa navyo vinatajwa kuhatarisha usalama wa watoto hasa wanapokuwa mbali na waangalizi.

Baadhi ya wakazi wa kata za Iganzo na Isanga,Six Mwasote na Ramadhan Kapichi walisema wapo baadhi ya wamiliki wa visima vya kuchimbwa wameendelea kuviacha wazi hatua waliyosema inaleta msukumo kwa viongozi hususani wenyeviti wa mitaa husika kuchukua hatua dhidi yao sawa na wanavyopaswa kufanya hivi sasa kuwahimiza wakazi wote kufukia madimbwi yaliyopo kwenye maeneo yao.

Kwa mujibu wa mtandao unaojihusisha na masuala ya haki za watoto wa www.sematanzania.org kwenye Moja ya Makala zilizochapishwa na mtandao huo April 8 mwaka 2016  Suala la ulinzi wa mtoto ni jukumu la jamii nzima, mlezi na mzazi mmoja mmoja kwa nafasi yake katika ngazi ya familia pamoja na serikali kwa ujumla.

Makala hayo yanaeleza kuwa Ushirikiano katika malezi ya mtoto kati ya wazazi, walezi pamoja na jamii unahitajika kwa kiwango kikubwa ili kuhakikisha usalama wa mtoto. Sehemu nyingine ya muhimu ni ushirikiano na mahusiano ya karibu kati ya mwalimu na mzazi ili kuhakikisha miendendo ya mtoto darasani, mtaani hadi nyumbani.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: