Mwenyekiti wa halmashauri ya Itigi mkoani Singida Ally Minja akitoa maelekezo wakati wa kikao cha baraza la madiwani 


Na Abby Nkungu, Singida

Serikali za Vijiji  katika  halmashauri ya Itigi mkoani Singida zimetakiwa kutenga maeneo na kuainisha matumizi bora ya ardhi kulingana na sheria zilizopo ili kupunguza migogoro miongoni mwa wananchi.

Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ally Minja wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika juzi kwenye ukumbi wa jengo jipya la makao makuu ya halmashauri hiyo mjini Itigi.

Minja alilazimika kutoa kauli hiyo kufuatia hoja mbalimbali za Madiwani kutaka Uongozi wa halmashauri hiyo kuingilia kati migogoro inayojitokeza mara kwa mara kwenye baadhi ya maeneo kutokana na watu wakorofi kuamua kujitwalia maeneo bila ridhaa ya viongozi wa vijiji husika.

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni diwani wa Kata ya Itigi Mjini aliwaambia Madiwani wenzake kwamba mamlaka ya kumruhusu au kumkataa mtu yeyote kuhamia katika eneo lao yapo mikononi mwa vijiji vyenyewe.

"Waheshimiwa Madiwani wenzangu, kutokana na ukweli huo, Mkurugenzi Mtendaji hahusika hata chembe na udhaifu wa kiutendaji unaotokea kwenye ngazi ya kijiji na hivyo kusababisha kero kwa wananchi" alitanabahisha Mwenyekiti Minja na kuongeza;

Kama kuna mtu kahamia kwa nguvu kwenye eneo lako, hilo sio la kumueleza Mkurugenzi Mtendaji. Nyie mna mamlaka kamili kumkubali au kumkataa kupitia vikao vyenu halali vya kijiji. Tabia ya baadhi yenu kuleta makao makuu ya halmashauri mambo madogo madogo ili kutaka kupatiwa ufumbuzi wake, haipendezi hata kidogo".

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, John Mgalula alipigilia msumari wa mwisho suala hilo akisema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya mwaka 1999 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002, ardhi ni mali ya kijiji; hivyo taratibu za matumizi yake yapo mikononi mwa wanakijiji wenyewe.

"Kutokana na Sheria hii, ni dhahiri halmashauri ya wilaya haipaswi kuja kuwalindia ardhi yenu wala kuingilia uamuzi wowote unaotolewa na Mkutano mkuu wa kijiji ambapo ninyi Madiwani ni Wenyeviti wake. Ninachoweza kuwasihi ni nyie kuhakikisha mnafuata sheria, taratibu na kanuni zote wakati wa vikao hivyo ili haki itendeke" alisema Mgalula.  

Awali, diwani wa Kata ya Aghondi, Jonas Msakuo aliomba uongozi wa halmashauri hiyo kwenda kumuonesha mipaka ya kata yake kwa kile alichodai eneo lake kuingiliwa na watu huku diwani wa Viti maalum, Rose Madumba akitoa angalizo juu ya uvamizi wa maeneo  na ujenzi holela katika kata ya Mitundu.

Naye, diwani wa Kata ya Ipande, Hamis Mwinje alitoa mwito kwa halmashauri hiyo kuanza kufikiria uwezekano wa kupima maeneo yote ya makazi ili wananchi wake waweze kujenga nyumba zilizo bora na za kudumu bila hofu ya kubomolewa na Mamlaka zilizopo madarakani.
Share To:

Francis Godwin Mzee wa matukiodaima

Post A Comment: