Na Shukrani Kawogo, Njombe.

Mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka amewapongeza walimu wawili wa shule ya msingi Nindi iliyopo wilayani Ludewa mkoani Njombe kwa juhudi wanazofanya kwa kuwafundisha wanafunzi wa shule hiyo kwa moyo wote bila kujali upungufu wa walimu walionao.

Walimu hao waliofahamika kwa majina ya Rebeca Mhagama Pamoja na Judith Kayombo wamekuwa wakifundisha wawili tu katika mikondo kumi na moja huku jumla ya wanafunzi wote ikiwa ni 308 wa shule ya msingi na 42 wa shule ya awali.

Pongezi hizo alizitoa alipofanya ziara ya siku moja kwa kutembelea miradi mbalimbali ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule hiyo pamoja na shule ya sekondari Chief Kidulile zilizopo wilayani humo.

“Hawa walimu wameonyesha moyo sana na wanawito wa kweli katika kazi hii, kwani kujitoa kufundisha wanafunzi wote hao wakiwa wawili tu na kufaulisha wanafunzi ni jambo ambalo linastahili pongezi za dhati kwao”, Alisema Ole Sendeka.

Walimu hao walifaulisha wanafunzi 24 kati ya wanafunzi 42 waliomaliza darasa la saba kwa mwaka jana na wanafunzi 40 kati ya 42 waliomaliza mwaka juzi.

Hata hivyo Ole Sendeka aliutaka uongozi wa idara ya elimu wilayani humo kutafuta walimu kwa haraka ili kuendeleza masomo ya wanafunzi kwakuwa walimu hao wote wawili wanatarajia kustaafu ambapo mmoja anastaafu mwezi wa sita na mwingine mwezi wa tisa mwaka huu.

Aidha kwa upande wa mmoja wa walimu hao Bi. Mhagama alisema kuwa pale shuleni wanakabiliwa na changamoto ya vyumba vya madarasa pamoja na ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa unaoendelea bado haviwezi kukidhi mahitaji yao kwani vyumba wanavyotumia sasa havifai kabisa kwa matumizi ya madarasa.

Alisema kuwa wanapata changamoto nyingi kuzungukia mikondo kumi na moja kuwafundisha wanafunzi hao na kusema kuwa angalau kidogo awali walipokuwa walimu watatu lakini mwenzao mmoja ni mgonjwa kwa muda wa mwaka mmoja na zaidi na kupelekea kubaki wawili kuendeleza masomo ya wanafunzi hao.

Aidha Ole Sendeka ameahidi kuwachangia shilingi mlioni moja kwa ajili ya kuongeza vyumba vya madarasa na kuwataka wananchi nao kuchangia ili vyumba hivyo viweze kuongezwa. 
Mkuu wa mkoa Christopher Ole Sendeka, akikagua ubora wa madarasa yaliyojengwa


Vyumba vya madarasa vikiwa vinaelekea kstika hatua ya mwisho ili vianze kutumika.

Mkuu wa mkoa wa njombe Christopher Ole Sendeka akimpongeza mwalimu Rebeca Mhagama kwa kazi nzuri anayofanya.(kutoka kulia ni mkuu wa wilaya ya Ludewa Andrea Tsere na wakwanza kushoto ni mwl. Judith Kayombo)
Share To:

Post A Comment: