Tuesday, 10 March 2020

Kampeni Ya Bukua Na Ushinde’ya Kampuni Ya ZOLA Yazinduliwa Dar Es Salaam


 1.Mkurugenzi Mkuu wa ZOLA ,Yusuph Nassoro, akiongea wakati wa hafla hiyo.
Meya wa Manispaa ya Ilala, Omari Kumbilamoto(kulia) akimkabidhi mmoja wa wanafunzi wa shule za sekondari zilizopo wilaya ya Ilala, Scolastica Thobias, zawadi ya madaftari baada ya kufanya vizuri katika mtihani wa mwisho wa mwaka jana 2019 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Bukua na Ushinde iliyoandaliwa na Kampuni ya umeme wa nishati ya jua ya ZOLA iliyofanyika patika viwanja vya Mnazi Mmoja.
Mkurugenzi wa Masoko wa ZOLA ,Eric Ballegu (kulia) akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari kutoka wilayani Ilala wakati wa uzinduzi huo.


Kunufaisha wanafunzi wakaofanya vizuri katika mitihani yao ya taifa

Kampeni ya kampuni ya ZOLA Electric Tanzania, ambayo zamani ilijulikana kama Mpower, inayolenga kuhamasihisha wanafunzi wa sekondari kusoma kwa bidii ijulikanayo kama ‘Bukua na Ushinde’ imezinduliwa wilayani Ilala jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Kupitia kampeni hii ambayo pia imelengakusaidia jamii na kuunga mkono jitihada za serikali kuboresha sekta ya elimu, ambapo itazawadia vifaa vya nishati ya umeme wa jua wanafunzi wa kidato cha nne watakaofanya vizuri kwenye mtihani wa Taifa wilaya humo mwaka huu, tayari kampeni hiyo imezinduliwa katika wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani. 

Akitangaza ofa hiyo katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja na kuhudhuriwa na wadau wa elimu na wanafunzi wa shule za sekondari ,Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya ZOLA, Yusuph Nassoro, alisema ‘Bukua na Ushinde’ imelenga kuchochea motisha kwa wanafunzi waliopo mashuleni kusoma kwa bidii ili waweze kufaulu mitihani yao vizuri hususani katika maeneo yenye changamoto ya nishati ya umeme kutoka gridi ya Taifa.

“Kampuni yetu tunaamini kuwa elimu ni ufunguo wa maisha na jamii ikielimika, inaweza kupiga hatua ya maendeleo kwa haraka,ndio maana tumekuja na mpango huu wa kutoa motisha kwa wanafunzi mashuleni, hususani maeneo yenye changamoto ya nishati ya umeme ikiwa ni moja ya sera yetu ya kusaidia jamii sambamba na kuunga mkono jitihada za serikali za kuboresha sekta ya elimu nchini”,alisema Nassoro.

Alisema wanafunzi watakaofanikiwa kuingia katika 10 bora katika mithani ya taifa ya majaribio watapatiwa zawadi ya vifaa vya kusomea na wanafunzi watatu watakaofanikiwa kuingia katika 3 bora watafungiwa mitambo ya umeme wa sola kwenye familia zao sambamba na kupatiwa vifaa vya kisasa vinavyotumia nishati hiyo kutoka kampuni ya ZOLA.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Ilala, Omari Kumbilamoto, ameipongeza kampuni ya Zola, kwa kubuni mpango huu wenye lengo la kuinua sekta ya elimu kupitia kutoa motisha kwa wanafunzi “Nawapongeza Zola kwa kuja na ubunifu huu ambao utachangia kuinua sekta ya elimu katika maeneo ya vijijini na mijini kwa kuwa umeme wa jua unaweza kutumika eneo lolote ”alisema.
Aliwataka wanafunzi kuendelea kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza ili ziwasaidie kupata mafanikio na kukamilisha ndoto zao na watambue kuwa kusoma kwa bidii na kupata maarifa ni moja ya njia itakayowapeleka katika kupata mafanikio katika Maisha yao sambamba na kutoa mchango wa kuendeleza Taifa.

Alimalizia kutoa wito kwa makampuni mengine ya biashara kusaidia huduma za kijamii zenye mwelekeo wa kuleta mabadiliko sambamba na kubuni biashara zinazochochea kuongeza fursa za ajira na kujiajiri kama ilivyo kampuni ya Zola.

Kampuni ya ZOLA Electric, ambayo zamani ilijulikana kama Mpower, ilianza kutoa huduma zake nchini mwaka 2012 ikiwa inatoa huduma za neshati ya umeme wa jua na kuuza vifaa vya kisasa vinavyotumia nishati hiyo.Hadi sasa bidhaa zake zinatawala soko nchini kwa asilimia 48%.

No comments:

Post a comment