Tuesday, 24 March 2020

DC MONDULI AFUNGA MNADA KISA MAAMBUKIZI YA COVID 19,wafanyabiashara wahaha

Sehemu ya shehena ya chakula Cha ngombe ikiwa sokoni kwenye Mnada wa Meserani kama ilivyokuwa na Kamera ya matukio eneo la Duka Mbuvu kata ya Meserani wilayani Monduli picha zote na Ahmed Mahmoud Arusha.

Wafanyabiashara wakiwa kwenye Mnada kabla ya kusitishwa na Mkuu wa wilaya hiyo eneo la Duka Bovu kata ya Meserani wilayani Monduli

Sehemu ya Mifugo ikiwa kwenye Mnada huo ulisitishwa huku wafanyabiashara wakirudi na mifugo yao majumbani zaidi ya Mifugo 3000 imekosa soko kutokana na kufungwa kwa Mnada huo kutokana na kuepuka maambukizi ya Covid 19 au virusi vya corona

Ngombe walioshiba ambao wametokana na uhimilishaji wanapatikana mnadani humo kama walivyokutwa na Kamera ya matukio wilayani Monduli.

Ngilisho,Arusha

Wafanyabiashara zaidi ya 1000 wa Ng'ombe katika Soko la Ng'ombe  mnada wa Meserani wilayani Monduli ,mkoani hapa wameshindwa kuuza mifugo yao mara baada ya mnada huo maarufu kufungwa kwa amri ya Mkuu wa wilaya ya Monduli,Iddy Kimanta kuzuia maambukizi mapya ya Corona.

Kufungwa kwa mnada huo kumelalamikiwa na wafanyabiashara wa Ng'ombe wakidai kwamba hawakupewa taarifa za kufungwa kwa mnada huo hivyo kusababisha athari kubwa kwao kwa kushindwa kuuza Ng'ombe zaidi ya 3000 zinazoletwa katika soko hilo maarufu kwa mnada wa Ng'ombe wilayani humo.

Wakizungumzia kadhia hiyo baadhi ya wafugaji na wafanyabiashara wa Ng'ombe , Zacharia Mollel na Andaskoi Saluni  wamedai kuwa walifika asubuhi katika soko hilo kwa ajili ya kuuza na kununua Ng'ombe lakini wameshangaa kukuta idadi kubwa ya askari polisi wakizuia kufanyika kwa mnada huo.

Mollel ambaye ni mfanyabiashara wa Nyama amesema kuwa amekuja katika mnada huo kununua Ng'ombe watano kwa ajili ya kuchinja lakini hatua ya kufungwa kwa mnada huo kumesababisha ashindwe kununua Ng'ombe kwa ajili ya biashara ya nyama.

"Mimi binafsi nanunua Ng'ombe watano katika mnada huu kwa ajili ya kuchinja ila ila kufungwa kwa mnada huu kutasababisha nikose Ng'ombe wa nyama jambo hilo kutapelekea kupanda kwa bei ya nyama   " Amesema Mollel.

Mfanyabiashara mwingine Andaskoi Saluni amesema kuwa ameshindwa kuuza Ng'ombe zake na kusababisha hasara kubwa ya kuwarejesha nyumbani na kuwachunga  kwani anaitegemea biashara hiyo kwa ajili ya kusomesha watoto wake na kuendesha maisha yake.

Akizungumzia kadhia hiyo Mkuu wa wilaya ya Monduli ,Iddy Kimanta amesema kuwa mnada huo umefungwa kwa sababu ya kuepusha msongamano wa maambuziki ya ugonjwa wa Corona.

Amesema kuwa mnada huo umefungwa kwa siku 30 na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kwa ajili ya kuepusha maambukizi mapya ya Corona kutokana na kwamba mnada unamwingiliano mkubwa na wafanyabiashara wa Ng'ombe kutoka nchi jirani ya Kenya.

Amewataka wafanyabiashara hao wa Ng'ombe kuwa wavumilivu hadi hapo serikali itakapotoa maelekezo  mengine.

*kamati ya ulinzi na usalama.ndio imefunga mnada huo ili kuepusha msongamano unaowez kusababisha maambukizo ya virusi vya Corona "Amesema Kimanta.
No comments:

Post a Comment