WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasi na Utalii wameitaka Serikali kutoa tuzo kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri kwa jitihada zake za upandaji miti katika eneo hilo.

Walisema kuwa ushiriki wake moja kwa moja na uhamasishaji wake katika jamii kuanzia Shule za Msingi hadi Vyuo Vikuu umesaidia kujenga uelewa wa umuhimu wa upandaji na utunzaji miti katika eneo hilo.

Mjumbe Kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kaliua Magdalena Sakaya alisema juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Tabora zimesaidia kuwaelimisha wanafunzi kutoka Shule za Msingi kujifunza umuhimu wa upandaji wa miti katika mazingira.

Alisema hatua hiyo imesaidia miti kuanza kuenea katika maeneo mbalimbali na kuondoa uwezekano wa Mkoa huo kugeuka jangwa.

Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini Flatei Massay alisema viongozi wengine ni vema wakaiga mfano huo ili waweze kuinusuru Tanzania kugeuka jangwa.

Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Chambani Yusuph Hussein alisema tafiti zinaonyesha kuwa kila mwaka kuna haribifu wa hekta 500,000 za miti na ambazo zinapandwa ni hekta 200,000 na zinazopona ni hekta 100.

Alisema ni vema viongozi mbalimbali wakaongeza juhudi katika upandaji miti na kulinda visiki vya miti iliyokatwa vising’olewe ili kurejesha uoto wa asili.

Hussein alisema jitihada za makusudi zinahitajika ili kuhakikisha miti mingi inapanwa na kuitunza na kudhibiti uharibifu wa mistu ili kuinusuru Tanzania isigeuke kuwa jangwa katika kipindi cha miaka michache ijayo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Kemerembe Lwota alisema wajumbe kwa kuridhika na juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Tabora katika suala zima la usimamiaji wa mazingira na upandaji miti wanaishauri Serikali kumpa tuzo.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuwahamasisha na viongozi wengine kuongeza juhudi katika suala zima la kulinda miti asili na kupanda mipya.

Lwota alisema kama Serikali itashindwa kutoa tuzo hizo wao watampatia tuzo kwa kutambua mchango wake aliounyesha wa upandaji miti mkoani Tabora.

Akijibu hoja za Wabunge, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Khamis Kigwangalla alisema kwa kutambua juhudi za Mkuu huyo wa Mkoa wanakusudia kumpa tuzo wakati wa maadhimisho ya wiki ya asili ambayo yatafanyika Kitaifa Mkoani humo mwezi Mei mwaka huu.

Alisema serikali itaendelea kuthamini na kutambua juhudi za wadau mbalimbali ambao wanashiriki katika uhifadhi wa mazingira na upandaji miti kwa ajili ya faida ya kizazi cha sasa na kijacho
 Waziri wa Maliasi na Utalii Dkt. Khamis Kigwangalla akitoa ufafanuzi juzi kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakipokuwa na ziara ya kikazi mkoani Tabora kukagua shughuli mbalimbali katika Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki(BTI).
 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalli Kemirembe Lwota( wa pili kutoka kushoto) akiongozana na wajumbe wa Kamati yake na Viongozi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki Tabora(BTI) kukagua shughuli mbalimbali wakati wa ziara yao ya kikazi juzi mkoani Tabora.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasi na Utalii kuhusu uhifadhi wa maliasi na upandaji wa miti katika Wilaya mbalimbali mkoani humo juzi wakati wajumbe hao walipokuwa na ziara ya kikazi Picha na Tiganya Vincen
Share To:

Post A Comment: