Friday, 13 March 2020

ATCL KUENDELEA KUTEKA SOKO LA SAFARI ZAKE TANZANIA-MUMBAI NA MWANDISHI WETU

SHIRIKA la Ndege Tanzania (ATCL) limeazimia kuongeza safari zake ili kuteka soko lake ikiwemo kwa wafanyabiashara wanaosafirisha  shehena za mizigo kati ya Mumbai na Tanzania.

Hatua hiyo itatekelezwa kupitia mkutano wa biashara uliofanyika hivi karibuni Mumbai nchini India kwa lengo la kukuza usafirishaji mizigo .

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo lililofanyika Jiji la Mumbai, Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda alieleza kuwa uhusiano wa wafanyabiashara wa Tanzania na India unatarajia kuwa mkubwa na masoko zaidi ya bidhaa zao kuongezeka.

Katika kongamano hilo zaidi ya Wafanyabiashara 130 walishiriki huku kati yao wafanyabiashara 30 kutoka Tanzania waliweza kuonyesha bidhaa zao ikiwemo za korosho, matunda, mbogamboga na mazao mengine ya kilimo
Pia bidhaa za plastiki, ufugaji, magari na teknolojia ambapo kwa pamoja waliweza kuonyesha na kujenga mtandao wa kibiashara.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa ATCL, Bwana. Patrick Ndekana alieleza kuwa  ATCL inafanya safari zake  za uhakika na salama kwa kumiliki ndege mpya za kisasa na mpya kabisa za Dreamlinner Boeing 787.

"ATCL tunaruka moja kwa moja kutoka Mumbai hadi Dar es Salaam ambapo pia ina ukubwa wa kubeba mizigo ya tani15.

Tunafanya safari katika maeneo mengine matano ya Afrika ikiwemo; Uganda, Burundi, Comoros, Zambia, Zimbabwe  na maeneo mengine."  Alieleza Bwana. Ndekana.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji mkuu wa Wafanyabiashara na Viwanda wa Indo-Afrika  Bi. Sunanda Rajendran  alipongeza juhudi za ATCL  kufikiia mafanikio yake huku wakiangalia namna ya kufanya kazi na shirika hilo.

"Tayari tunafanya kazi na nchi ya Ethiopia  na Kenya.  Kwa sasa tunaangalia namna ya kufanya kazi pamoja na Tanzania.

Ushirikiano baina ya nchi mbili utaleta mwanzo mzuri nawahakikishia kushirikiana na 'Air Tanzania". Alisema Bi. Sunanda Rajendran

ATCL  yenye makao yake makuu Jijini Dar es Salaam uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Lilianzishwa tangu mwaka 1977  na limekuwa mwanachama wa Shirika la Ndege la Afrika (The  African Airlines Association-AFRAA).

ATCL ni miongoni mwa mashirika makubwa likiwa na ndege zake mbalimbali zikiwemo Bombardier DASH8 Q400.

Pia ndege mbili za Airbus A220-300 na moja Boeing 787 Dreamliner na nyinginezo.


No comments:

Post a comment