Na Jacquiline Mrisho -  MAELEZO
Serikali ya Israel imeikabidhi rasmi Tanzania Kitengo cha Magonjwa ya Dharura na Majeruhi (TRAUMA UNIT) kilichopo katika Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo jijini Dodoma


Makabidhiano hayo yamefanyika jana jijini Dodoma baina ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge na Naibu Balozi wa Israel nchini Tanzania, Eyal David baada ya kumaliza kuweka miundombinu, vifaa tiba na kutoa mafunzo kwa wataalam wa afya watakaotoa huduma katika kitengo hicho.

Dkt. Mahenge ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika tukio hilo, amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt, John Pombe Magufuli aligawa viwanja vilivyopo jijini Dodoma kwa Taasisi mbalimbali za Kimataifa hivyo kukiwa na huduma dhaifu za afya hakuna taasisi yoyote ya kigeni itakayokuwa tayari kuleta watu wake.

“Kutokana na uwepo wa Kitengo cha Magonjwa ya Dharura na Majeruhi chenye huduma zenye hadhi ya kimataifa katika hospitali hii kunaifanya Serikali kujiamini katika kuitangaza nchi kimataifa hasa kukaribisha wageni kuja kuwekeza na kufanya shughuli mbalimbali ndani ya jiji hili”, alisema Dkt. Mahenge.

Kwa upande wake Naibu Balozi wa Israel nchini Tanzania, Eyal David amesema kuwa afya ni sekta muhimu kati ya sekta kubwa ambazo wana ushirikiano nazo hivyo mradi huo ni ushirikiano wa kisekta baina ya nchi hizo mbili.

“Serikali ya Israel kupitia shirika lake la Maendeleo la MASHAV lilitoa msaada wa kujenga miundombinu na kuweka vifaa tiba ambavyo vimegharimu takriban shilingi bilioni 2.2, hii yote ni njia moja wapo ya kuboresha mahusiano yetu pamoja na kuboresha sekta ya afya nchini Tanzania”, alisema Naibu Balozi, Eyal.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, Dkt. Alphonce Chandika amesema kuwa palipo na msongamano wa watu magonjwa ya dharura hayaepukiki hivyo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuamua kukiweka kitengo hicho jijini Dodoma kwani jiji hilo linategemewa kuwa na ongezeko la watu kwa kiasi kikubwa.

“Sote tunafahamu kuwa wagonjwa wa dharura wasipopata huduma ndani ya muda fulani kuna uwezekano mkubwa wa kupata madhara zaidi ikiwemo ulemavu wa kudumu au kupoteza maisha hivyo huduma hizo ni za muhimu, na kwa hospitali hii huduma zinazopatikana ni sawa na utakazozipata nchi zingine ikiwemo Israeli”, alisema Dkt. Chandika.

Mnamo Januari 22, 2018 Serikali ya Tanzania na Israel ziliingia makubaliano ya kuanzisha kitengo hicho katika hospitali hiyo ambapo hadi sasa jumla ya wagonjwa 3000 wamehudumiwa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: