Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida,  Edward Mpogolo (kulia) na Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Justice Kijazi wakipanda miti  katika maadhimisho ya siku ya upandaji miti yaliyofanyika kiwilaya Kijiji cha Nkhoiree Kata ya Iseke Tarafa ya Ihanja jana.
  Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida,  Edward Mpogolo (kulia) na Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Justice Kijazi wakizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Nkhoiree kabla ya uzinduzi wa maadhimisho hayo.
 Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Justice Kijazi, akizungumza
 Msafara wa kwenda kupanda miti.
  Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida,  Edward Mpogolo, akizungumza.
 Miti ikipandwa.
Mkutano wa uzinduzi ukifanyika.

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKUU wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Edward Mpogolo amepiga marufuku uchomaji wa mkaa na uvunaji wa mbao katika wilaya hiyo bila kufuata taratibu za uvunaji wa miti kama GN No. 417 ya Mwaka 2019 inavyo elekeza.

Mpogolo alipiga marufuku vitendo hivyo juzi katika maadhimisho ya siku ya upandaji miti yaliyofanyika kiwilaya Kijiji cha Nkhoiree Kata ya Iseke Tarafa ya Ihanja ambapo miti 500 ilipandwa.

Katika hatua nyingine Mpogolo amewataka viongozi wote wa vijiji kuwa mstari wa mbele kuhifadhi mazingira katika maeneo yao kwani Ikungi ya miaka 2000 ilikuwa na miti na wanyama na sasa hali inazidi kuwa mbaya na sisi viongozi na wakala TFS tupo tunaona.

" Nimewaomba Wakala wa Huduma za Misitu(TFS) kuchunguza na kuwachukulia hatua baadhi ya watendaji wao wasio waaminifu. Ninawaalika waje huku vijijini tufanye mikutano ya hadhara wasikie kilio cha wananchi dhidi ya utolewaji wa vibali usio halali vya usafirishaji wa mazao ya misitu" alisema Mpogolo.

Alisema  wananchi wanalalamika kutunza na kuhifadhi misitu yao lakini baadhi ya watendaji wasio waaminifu wa TFS wanatoa vibali bila kufuata taratibu ambazo wao wenyewe wamejiwekea kwenye sheria (The Forest Regulation, 2019).

Mpogolo amewahimiza pia kila nyumba kuwa na mizinga ya nyuki isiyopungua mitatu kwani kufuga nyuki kunahifadhi mazingira kama sheria ya Uhifadhi ya Nyuki ya Mwaka 2002 inavyoelekeza. Aidha alisema kufuga nyuki kunaongeza kipato kwa kuuza asali ambapo mzinga mmoja unaweza kupata zaidi ya sh. 200,000/= kwa mwaka. 

Ameahidi kuwapeleka kwenye mafunzo vikundi vya vijana vitakavyokuwa tayari kufuga nyuki ambapo hadi sasa vijana watatu kutoka Kata ya Issuna wanahudhuria mafunzo ya mwezi mmoja.

Mkurugenzi wa wilaya hiyo Justice Kijazi alisema  lengo la upandaji miti kwa mwaka wa fedha 2019/ 2020 ilikuwa ni kupanda zaidi ya miti 500,000 ambapo mpaka kufikia jana jumla ya miti 280,000 ilisambazwa na kupandwa na zoezi la usambazaji wa miche hiyo linaendelea.

Kijazi alisema miti iliyokwisha kupandwa watu binafsi wamepanda miti 208,000, shule za msingi 37,000, shule za sekondari 20,000 na Taasisi mbalimbali miti 15,000.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: