Monday, 10 February 2020

Canada Yatoa Bilioni 90 Kuboresha Elimu Ya Ualimu


Na Ferdinand Shayo,Arusha.

Nchi ya Canada imetoa bilioni 90 kwa Tanzania zitazotumika kuboresha elimu ya ualimu nchini na kuwezesha kuinua kiwango cha ubora wa elimu katika shule za msingi na sekondari hivyo kuzalisha rasilimali watu yenye ubora wa hali ya juu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Dr.Leonard Akwilapo katika kikao kazi cha kupitia na kutathmini utekelezaji wa mradi  wa kuendeleza elimu ya ualimu nchini (TESP) ,ambapo amesema kuwa Canada imetoa fedha hizo ambazo zimetumika katika kujenga vyuo vipya vya ualimu,kuboresha miundombinu ya kufundishia pamoja na mafunzo ya ualimu.

Dr.Leonard amesema kuwa Ushirikiano wa Tanzania na Canada unalenga kuongeza uwezo wa vyuo vya ualimu kufundisha walimu waliobobea watakaofundisha vizuri katika shule mbalimbali.

“Tunatoa shukrani nyingi sana kwa serikali ya Canada na kitengo chao cha Global Affairs ambacho kinasimamia mradi huu,mafanikio makubwa yamepatikana kupitia mradi huu na matokeo yameshaanza kuonekana walimu wameongeza uwezo katika ufundishaji” Anaeleza Dr.Leonard

Kansela Mkuu ,Ushirikiano na Maendeleo  Canada  ,Gwen Walmsley amesema kuwa Canada itaendelea kutoa fedha zaidi katika kuboresha sekta ya elimu nchini na mradi huo ni moja kati ya juhudi wanazozifanya katika kuunga mkono serikali ya Tanzania kuboresha elimu.

Gwene anasema kuwa nchi ya Canada imefanikiwa kuwa moja kati ya nchi zenye elimu bora duniani kutokana na kuwekeza kwa walimu  na kuhakikisha maslahi bora ya walimu .

Mratibu wa Mradi wa kuendeleza Elimu  ya Ualimu kwa Walimu ,Ignas Chonya amesema kuwa mradi huo umewawezesha walimu kuboresha mbinu za ufundishaji kupitia Tehama ambapo vyuo 35 vya ualimu vimeanganishwa na mfumo huo na wanatarajia kuunganishwa na mkongo wa taifa.

No comments:

Post a comment